Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2021 01 13Article 521021

Siasa of Wednesday, 13 January 2021

Chanzo: HabariLeo

Chanzo cha mwanahabari Selina Wilson kuingia katika siasa

Chanzo cha mwanahabari Selina Wilson kuingia katika siasa

KUNA stori mmoja mashuhuri kuhusu wanawake na siasa za Tanzania. Ni hadithi inayohusu mazungumzo yaliyofanywa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, na mmoja wa wapigania uhuru mashuhuri nchini, Hayati Bibi Titi Mohamed.

Baada ya Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961, Nyerere aliunda Baraza la Mawaziri la Kwanza na hakukuwa na mwanamke aliyeteuliwa kuwa waziri kamili. Jambo hilo linadaiwa kuwa lilimkera Titi.

Mwanamke huyo akamfuata Mwalimu Nyerere na kumhoji ni kwa vipi wanawake wamenyimwa nafasi ya kuwa mawaziri kamili na badala yake kupewa nafasi za unaibu waziri pekee. Nyerere akamjibu kwamba amepata shida kupata wanawake “wenye sifa stahiki” ili awateue kuwa mawaziri.

Kwa mujibu wa stori hiyo, Titi akamuuliza Mwalimu: “Hao wanaume walio na sifa leo, walikuwa wapi wakati tukipigania Uhuru?” Titi alikuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kudai uhuru.

Kwa mujibu wa mwanahistoria wa mapambano ya kudai Uhuru wa Tanganyika, Mohamed Said, kuondoa Mwalimu, hakukuwa na mwanasiasa mwingine mashuhuri nchini aliyemzidi Titi Mohamed wakati ule.

Yeye ndiye aliunganisha wanawake na Watanganyika kwa jumla katika mapambano ya kudai uhuru na mara zote akipanda jukwaani kabla ya Mwalimu Nyerere kuzungumza kwenye mikutano ya hadhara.

VITI MAALUM

Baada ya uamuzi huo wa Mwalimu wa mwaka 1961, ilichukua miongo miwili kwa Tanzania kupata mbunge wake wa kwanza wa kuchaguliwa.

Kwa miaka yote ya 1960 na 1970, wabunge wote wanawake waliokuwa bungeni waliingia kwa utaratibu wa viti maalumu. Katika kesi maarufu ya Martha Wejja dhidi ya Kitwana Kondo katika miaka ya 1980, mwanamama huyo alishinda kesi baada ya kuthibitisha kuhusu maneno ya kejeli na udhalilishaji yaliyofanywa dhidi yake na mshindani wake kwa sababu yajinsia yake.

Baada ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yaliyotokea mwanzoni mwa miaka ya 1990 -ukijumuisha na Mkutano wa Beijing kuhusu uwezeshaji wa wanawake, taratibu ‘kibao kilianza kugeuka.

’ Kwanza, kuruhusiwa mfumo wa vyama vingi kulimaanisha kutanuka kwa wigo wa wanawake kuwania nafasi za uongozi kupitia vyama vingine vya kisiasa.

Zaidi ya chama tawala cha CCM, wanawake sasa walijitokeza kuwania nafasi katika vyama vya upinzani na kupata fursa ambazo zisingekuwa rahisi kuzipata katika mfumo wa chama kimoja.

Kuruhusiwa kwa asasi za kiraia pia kulifungua njia kwa wanawake kuonesha uwezo, maono na ujasiri wao kwenye kuhoji na kuishauri serikali kwenye mambo ya maslahi kwa taifa.

Mwaka 2010, Tanzania ilipata wanawake wabunge 23 waliopata nafasi zao kupitia majimbo ya uchaguzi.

Ukijumuisha na wale wa viti maalumu, Bunge la Tanzania likafikisha asilimia 29 ya wabunge wanawake -kiwango cha juu kabisa kwa wakati huo.

Si tu bungeni, bali hata katika nafasi mbalimbali kama za udiwani, ujumbe wa halmashauri kuu na nafasi nyingine za kisiasa; wanawake walipata mwamko mkubwa na kuwania nafasi. Selina Wilson ni miongoni mwa mwanahabari waliobobea kuandika habari za siasa kupitia Gazeti la Uhuru linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Naye alijitosa kwa mara ya kwanza kuwania udiwani wa viti maalum mkoani Pwani mwaka 2010 baada ya kupata ushawishi mkubwa kutokana na kushuhudia uendeshaji wa mabaraza ya madiwani na kuwaona baadhi ya madiwani wakishindwa kutetea maslahi ya wananchi.

Akizunguma na HabariLEO, Selina ambaye kwa sasa ni Diwani wa Viti Maalumu mkoani Pwani anasema: “Kilichonivutia na kunifanya niingie katika siasa, ni kero za wananchi maana nilikuwa naenda kuripoti vikao vya baraza la madiwani.

” Anasema huko alibaini kuwa “Kuna hoja zinazotolewa unaona kabisa hii ni ‘hot’ sasa tunataka madiwani wapambane waibane serikali itekeleze jambo fulani, lakini unakuta diwani anasimama anasema naunga mkono hoja, kitu ambacho unakiona kabisa anapaswa kusimama na kupinga kwa hoja makini ili kutafuta ufumbuzi makini.

” Anasema: “Hicho kitu kilikuwa kinanikera sana, nikajiuliza diwani anatakiwa aweje? Awe na sifa gani, nikaanza kufuatilia hiyo ilikuwa mwaka 2007.

Nikawa naulizia ulizia, nikambiwa diwani anatakiwa awe mfuatiliaji wa kero za wananchi na kuzitafutia majawabu.

” Mwanahabari huyo anasema kingine kilichomkera ni mikopo ya kina mama na vijana asilimia 10 ambayo kwa sasa inawahusisha pia watu wenye ulemavu.

Selina anasema: “Unakuta mnasomewa bajeti ya Sh bilioni 1.3, ukipiga hesabu kwa asilimia 10 inaenda kwenye Sh milioni 100, lakini unakuta Halmashauri ya Kibaha inatenga Sh million tano au nane na ukienda kwenye vikao, unakuta hawaulizi wala hawatetei…” Anasema: “Kwa kweli nilikuwa najiuliza madiwani wanakuwaje; wanakutana na nini kwenye vikao vyao vya ndani, mbona wakija kwenye vikao vya baraza wanapoa, nikasema ngoja nigombee nione inavyokuwa.

Mwaka 2010 nikagombea nikiwa mwandishi tu wa kawaida, sikuwa na fedha zozote za kuwazungukia wajumbe kifupi sikuwa na kitu.” Kwa mujibu wa Selina, ajenda zake kuu zilikuwa mbili.

Kwamba, kama atachaguliwa, basi aende kuhakikisha kweli asilimia 10 inatengwa asilimia 10 maana ile ya milioni nane wakiomba milioni tatu, wanapewa 300,000 matokeo ya mikopo yakawa hayaonekani kwenye vikundi.

Anasema: “Nilipojenga hoja hiyo, wanawake wakanikubali. Nilijenga hoja nyingine kuhusu huduma za jamii maana kulikuwa na changamoto nyingi kwa wanawake hususani katika suala la huduma za afya hasa katika zanahati kwani wanawake wanatembea umbali mrefu, kitu hicho kilikuwa kinanikereketa sana.

” Katika mazungumzo na HabariLEO, Selina anasema katika kipindi hicho, Tanzania ilikuwa inatekeleza malengo ya maendeleo ya milenia.

“Kutokana na uandishi wangu wa habari, nilipata mafunzo kutoka UN (Umoja wa Mataifa) kuhusu namna tunavyopaswa kupiga kelele kuhakikisha wanawake wanajifungua salama na kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na wajawazito ili kutekeleza Lengo la Nne na la Tano la Malengo ya Maendeleo ya Milenia,” anasema.

“Nashukuru katika uchaguzi ule wa 2010, kwa mara ya kwanza nilishinda, na nilipoingia tu madarakani, namshukuru Mungu nikashirikiana na wenzangu kuhakikisha tunapandisha kiwango cha mikopo ya kina mama na vijana, kutoka Sh milioni nane mpaka Sh milioni 15 baadae tukafikisha Sh milioni 30 hadi 2015 tulifanikiwa kutenga milioni 300,” anasema.

Anaongeza: Ndiyo maana hivi sasa ukisema unataka kukutana na akina mama tuliowapa mikopo, utakutana na umati mkubwa wa watu, na wengi wamefanikiwa kubadilisha maisha yao.

” MIKOPO YA VIJANA

Selina anasema kutokana na vijana kusuasua katika urejeshaji wa mikopo, katika Serikali ya Awamu ya Tano wamekuja na njia mbadala za kuwabana kwa kuanzisha chama cha kuweka na kukopa (Saccoss) maalum ya vijana.

“Ukiwapa mikopo inasumbua hivyo tumeamua kuwapa mikopo kupitia Saccos, ili kijana apate mkopo, lazima awe mwanachama, hata hivyo haifanyi vizuri sana hivyo tumekuja na mbinu mpya ya kuwapa vifaa.

Mfano, anayehitaji mkopo wa bodaboda tunamnunulia bodaboda, mama lishe tunawanunulia vifaa na mahitaji yote,” anasema Selina ambaye ni mwanahabari na mwanasiasa nguri.

CHANGAMOTO

Anasema: “Wakati naanza, nilipata upinzani mkubwa kwa viongozi na madiwani wengine ambao waliona si vema waandishi wa habari kuingia kwenye siasa, walikuwa wanasema waandishi wa habari wakiingia humu watatusumbua na kuanza kutuhoji hoji, haiwezekani kuwa na diwani mwandishi wa habari, hata hivyo nashukuru pamoja na vita kubwa iliyokuwepo, nilifanikiwa kuvuka kihunzi hicho na sehemu kubwa ya ahadi yangu nimetekeleza.

” Selina anasema anajipanga ili mwaka 2025 iwapo Mungu atamjalia afya njema na uzima, basi ajitose kuwania ubunge na kupandisha viwango vyake vya siasa. KUPUUZA YANAYOKATISHANA TAMAA “Kuna misemo ya kuvunja moyo wanawake ili wasigombee nafasi mbalimbali za uongozi katika siasa; kwa kweli nawashauri wanawake wenzangu wote tuipuuze.

Hii ni misemo ya ovyo kama adui wa mwanamke ni mwanamke maana haina ukweli wala uhalisia wowote wa uadui baina ya mwanamke na mwanamke, badala yake tuendelee kushikamana na kuungana mkono katika mambo yetu,” anasema Selina.

Anasema mada kuhusu jinsia inaeleza tofauti za kimajukumu kati ya mwanaume na mwanamke na wakati mwingi katika jamii, wigo wa kisiasa unaaminika kuwa ni wa mwanaume pekee jambo ambalo si kweli kwani siasa na uongozi ni haki na jukumu la wote.

“Zipo aina nyingi za kuvunjwa moyo si tu kwa misemo hiyo, bali pia hata kwa kukatishwa tamaa kwa kunyanyaswa, kudhalilishwa, kutolewa habari au taarifa za kuvunja moyo kwenye mitandao ya kijamii, hivyo wanawake tusivunjike moyo wala tusitorudi nyuma hadi tuhakikishe tunatimiza malengo yetu,” anasema. Anaongeza: “Msemo wa adui wa mwanamke ni mwanamke, usipewe nafasi kuwagawa wanawake katika siasa na uongozi kwani sababu ni msemo wa kisiasa usio na mantiki,” anasema.

Anasema, msemo huounalenga kuwatenganisha wanawake na kufanya nguvu yao kuwa chini ili wakose nafasi katika uchaguzi kutokana na fursa ya uwingi wao unaowaogopesha baadhi ya wanaume na kuwafanya kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo misemo isiyo na ukweli ili kuwadhoofisha.

Join our Newsletter