Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2021 01 09Article 520826

xxxxxxxxxxx of Saturday, 9 January 2021

Chanzo: habarileo.co.tz

‘Deni kura za JPM litalipwa kwa maendeleo’

MBUNGE wa Jimbo la Bariadi mkoani Simiyu, Kundo Mathew, amesema kura za wananchi wa Bariadi kwa Rais John Magufuli ni deni litakalolipwa kwa kuwaletea maendeleo kwa kasi kubwa.

Kundo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza vijana wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wa Wilaya ya Bariadi baada ya kushiriki uchimbaji msingi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya katibu wa umoja huo.

Akiwa katika kazi hiyo, Mbunge huyo alichangia mifuko 100 ya saruji na kuahidi kuongeza mifuko mingine 50 ya saruji pamoja na kutoa mabati yote yatakayohitajika kuezeka nyumba hiyo.

“Rais Magufuli ametoa mwelekeo wa nini cha kufanya, kura za wananchi zitalipwa kwa kuwaletea maendeleo… Mmetukopesha kura pamoja na Rais wetu Magufuli; wajibu wetu ni kuwaletea maendeleo... Mambo mengi yanatuhitaji jimboni kazi kubwa ni moja ya kutekeleza miradi yenye tija kwa maendeleo ya Bariadi,” alisema Kundo.

Alisema chama na jumuiya zake zitajengwa kwa kujitolea hivyo, akawataka wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia kwa hali na mali ujenzi wa ofisi za kata, wilaya na Mkoa wa Simiyu.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, vijana wa UV-CCN wanapaswa kuwa imara zaiodi kwani vijana legelege, watakifanya chama kuwa legelege.

“Wote katika katiba ya CCM tuna haki sawa na ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuna haki sawa; ukiwa unajiamini na kutekeleza Ilani ya CCM, acha wadau waje kuchangia maendeleo... Huku ni nyumbani kwetu tusitie aibu kukuta mazingira si bora,” alifafanua Kundo.

Alisema baada ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya katibu wa vijana atahakikisha unaanza ujenzi wa ofisi za makatibu kata 31 ili kujenga heshima ya Chama Cha Mapinduzi ili madiwani na makatibu kata wapate mahali pa kutunza mafaili yao pamoja na kuwa na sehemu ya kukutana na wanachama.

Kundo aliitaka Jumuia ya Umoja wa Vijana katika Wilaya ya Bariadi, kushirikiana katika ujenzi wa ofisi za chama kwa ngazi zote ikiwemo za kata, wilaya na mkoa.

Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Khamis Magohe, alimpongeza Naibu Waziri Kundo kwa kutimiza ahadi ya mchango wake pamoja na kushiriki uchimbaji wa msingi.

Magohe aliwataka wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kuchangia ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi wa CCM ili wawe na makazi bora na ofisi nzuri ili huduma zitolewe kwa kiwango na ubora kinachotakiwa.

“Tunashukuru sana kwa mchango wako na wadau wengine waliokwishajitokeza kutuchangia... Tunawaomba na wengine waigie na waje kuchangia ili kuimarisha makazi na ofisi za chama tukilenga kutoa huduma bora na kwa wakati.” alisema Magohe.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Kitebo Kulwa, alisema lengo la michango hiyo ni kuimarisha chama na jumuiya zake. Aliwataka wadau wengine kujitokeza kwa wingi kuchangia shughuli za CCM.

“Katika kutekeleza Ilani ya CCM, Mbunge wetu Kundo tayari ameshachimba na kuweka pampu za maji kwenye visima vitatu katika Kata za Nkololo, Mwaumatondo na Ihusi na pia, ameanza kufungua mawasialino ya barabara kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za mjini na Vijijini (Tarura),” alisema Kitebo.

Join our Newsletter