Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 09 25Article 510268

Siasa of Friday, 25 September 2020

Chanzo: HabariLeo

Dk Mwinyi awaahidi neema machinga

Dk Mwinyi awaahidi neema machinga

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, amesema akichaguliwa kuongoza Zanzibar anakusudia kujenga mazingira mazuri kwa wafanyabiashara ndogo (machinga), ili watambuliwe rasmi na kuepuka kusumbuliwa.

Alitoa ahadi hiyo wakati alipotembelea wafanyabiashara katika soko la Kwa Hajitumbo na wanaofanya biashara za nguo na vitambaa katika eneo la Pindamgongo, eneo la Saateni, Unguja jana.

Alisema amefurahishwa na vijana wengi kuitikia wito wa kujiajiri kwa kufanya biashara ambazo zinawaingizia kipato na kuendesha maisha yao.

“Kama nitapewa ridhaa ya kuongoza Zanzibar nakusudia kujenga mazingira mazuri ya biashara kwa vijana, ikiwamo kusogeza huduma mbalimbali za miundombinu ya fedha kama taasisi za kibenki.”

“Nimefurahishwa na juhudi zenu za kujiajiri katika eneo hili la Saateni, nikichaguliwa nataka kuimarisha miundombinu ambayo itawawezesha kufanya biashara vizuri na kuingiza kipato zaidi,” alisema.

Baadhi ya wafanyabiashara katika soko hilo, walimweleza mgombea huyo wa urais kuwa, ukosefu wa miundombinu mizuri, kwa kiasi kikubwa kunachowafanya washindwe kufanya biashara vizuri.

''Tunaziomba taasisi zinazohusika ikiwamo Baraza la Mji kututambua wafanyabiashara wadogo kama wanavyofanyiwa wenzetu wa Tanzania Bara, ili tufanye biashara zetu vizuri na kulipa kodi serikalini pamoja na kuondoa usumbufu,'' alisema Abrahman Ali Daudi.

Mfanyabiashara mwingine, Aboud Said, aliliomba Baraza la Manispaa kusogeza huduma nyingine ikiwamo biashara za aina mbalimbali ambazo zitawafanya wananchi wengi ikiwamo wateja kufika eneo hilo.

''Tunaiomba Manispaa ya Mji kuligeuza eneo hili la biashara na kuruhusu kuwapo biashara mchanganyiko, ambazo zitawawezesha wananchi kufika kwa ajili ya kufanya biashara na manunuzi,'' alisema.

Dk Hussein Mwinyi amejiwekea utaratibu wa kufanya ziara na kuonana na wananchi ana kwa ana katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba kwa ajili ya kujua matatizo yao ili akichaguliwa aweze kuyatatua.

Join our Newsletter