Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2021 01 14Article 521090

Siasa of Thursday, 14 January 2021

Chanzo: HabariLeo

Kamati za Bunge kuanza vikao Januari 18

Kamati za Bunge kuanza vikao Januari 18

KAMATI za Kudumu za Bunge la Tanzania zitaanza vikao Januari 18 hadi 31 mwaka huu jijini Dodoma kutekeleza majukumu ya kibunge kabla ya Mkutano wa Pili wa Bunge la 12 unaotarajiwa kuanza Februari Pili mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha Bunge, jijini humo ilionesha kuwa, pamoja na uchaguzi wa viongozi wenyeviti na makamu wenyeviti pia wajumbe wa kamati hizo watapewa mafunzo kuhusu utendaji wa kamati za Bunge na mfumo wa Bunge la Jumuiya ya Madola.

Taarifa hiyo inaonesha mafunzo yatakayotolewa ni ya kuhusu majukumu na taratibu za uendeshaji wa kila kamati, kuhusu Bunge mtandao na usalama wa mtandao kwa kamati zote na pia kuhusu kamati za kisekta zinazopokea maelekezo ya wizara kuhusu muundo, majukumu ya taasisi na sera na sheria zinazosimamiwa na wizara hizo.

Ilisema wabunge hao pia watapewa mafunzo kuhusu Kamati za Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) na Kamati ya Bajeti kuhusu uchambuzi wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Msajili wa Hazina (TR) na namna bora ya kuhoji maofisa masuuli.

Pia wabunge hao watapewa mafunzo kuhusu Kamati ya Sheria Ndogo namna inavyofanya kuhusu shughuli za uchambuzi wa sheria hizo, pia kuhusu uzoefu wa mabunge mengine ya nchi zinazofuata mfumo wa kibunge wa Jumuiya ya Madola.

Katika kipindi hicho Kamati ya Bajeti itapokea na kujadili taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa pili wa Maendeleo ya Taifa ya miaka mitano (2016/17-2020/21).

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/22-2025/26) pamoja na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka mmoja 2021/22.

Pia itapokea na kujadili mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali pamoja na sheria ya Fedha kwa kipindi cha nusu mwaka, kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Taarifa hiyo inaonesha kwamba vikao vya kamati hizo vinafanyika kabla ya Mkutano wa Pili wa Bunge la 11 kuanza ambao uliopangwa kuanza Februari 02, mwaka huu.

Join our Newsletter