Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 21Article 519755

Siasa of Monday, 21 December 2020

Chanzo: HabariLeo

Lipumba afufua madai ya katiba mpya, tume huru

Lipumba afufua madai ya katiba mpya, tume huru

MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amedai suala la Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi ni muhimu kwa sasa, ili kuleta demokrasia ya kweli nchini na kuondoa makandokando yaliyojitokeza katika uchaguzi mbalimbali ukiwemo wa Oktoba 28 mwaka huu.

Akizungumza katika kongamano maalumu, lililondaliwa na chama hicho kwa ajili ya kukusanya maoni ya wanachama na wananchi kwa ajili ya kupata maoni juu ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, Profesa Lipumba alisema vitu hivyo viwili vinaendana kwa pamoja katika kuleta haki.

"Hili siyo suala tuliloanza kulidai kuanzia jana wala juzi, sote tumeona mambo mengi yaliyotokea katika uchaguzi huu ikiwemo haki za vyama na wagombea wetu kudhulumiwa, haya yote kama tungekuwa na katiba bora yasingetokea,"alisema.

Alisema kukosekana kwa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, kunatoa fikra pevu kwa wananchi kuwa na fursa ya kuwapata viongozi wanaowataka bila kulazimishwa na mfumo.

Naye mchokoza mada katika mkutano huo, Wilfred Rwakatare, alisema siyo mara ya kwanza kwa chama hicho kuanzisha vuguvugu la kudai katiba mpya, kwani hata huko nyuma walianzisha vuguvugu hilo chini ya Dk Sengondo Mvungi, aliyefariki miaka ya karibuni.

Alisema hadi sasa chama hicho kimerudi tena kuwaamsha wananchi juu ya suala hilo, ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Alisisitiza kuwa katiba mpya na tume huru ni muhimu ili kukabiliana na CCM.

Alisema vyama vya upinzani, pia vina udhaifu mwingi ikiwemo ya usaliti miongoni mwa viongozi wa vyama hivyo, jambo linaloifanya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kupata nguvu ya kutawala wakati wote.

Join our Newsletter