Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 10 29Article 513400

Siasa of Thursday, 29 October 2020

Chanzo: HabariLeo

MIAKA 25 YA MSOTO, HATIMAYE CCM YAKOMBOA JIMBO

MIAKA 25 YA MSOTO, HATIMAYE CCM YAKOMBOA JIMBO

TANGU historia ya Vyama vingi ihasisiwe nchini,mwaka 1992 na kufanya uchaguzi wake wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 kwa mara ya kwanza jimbo la Moshi Mjini limechukuliwa na Chama tawala (CCM).

Historia inaonyesha uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995, Jimbo la Moshi lilichukuliwa na Joseph Mtui wa NCCR-Mageuzi na baadae akaja hayati Philemon Ndesamburo (2000-2015) na kurithiwa na Jaffar Michael wa Chadema pia na kulifanya jimbo hilo kuwa ngome kuu ya Chadema kwa miaka 20.

CCM ambayo ilikuwa ikiliwinda jimbo hilo kwa miaka 25, imeandika historia mpya kwa kuivunja ngome hiyo baada ya mgombea wake Priscus Tarimo kuibuka kidedea dhidi ya wapinzani wake.

Katika matokeo yaliyotangazwa leo Oktoba 29,2020 na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Michael Mwandezi, mgombea ubunge wa CCM, Priscus Tarimo ameibuka na ushindi kwa kupata kura 31,169 huku mshindani wake wa karibu, Raymond Mboya wa Chadema akipata kura 22,555.

Mwandezi alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, jimbo la Moshi mjini lilikuwa na wapiga kura walioandikishwa 143,267 na waliopiga kura walikuwa 54,994 ambapo kura halisi zilikuwa 54,386 na kura 608 ziliharibika.

Wagombea wengine wa ubunge katika jimbo hilo na kura zao zikiwa kwenye mabano ni Buni Ramole wa ACT-Wazalendo (374), Issack Kireti wa SAU(93), Fatuma Msuya wa Cuf (85), Dkt Godfrey Malisa wa NCCR-Mageuzi (59) na Neema Mushi wa Demokrasia Makini (51).

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Priscus aliahidi kwenda kutekeleza ahadi mbalimbali za maendeleo alizozitoa kwa wananchi wa jimbo hilo na kuwashukuru wapiga kura wa jimbo hilo kwa kumwamini na kumpa ridhaa.

Join our Newsletter