Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 19Article 519485

xxxxxxxxxxx of Saturday, 19 December 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Mabaraza ya madiwani yatakiwa kujadili changamoto za walemavu

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga ameyataka mabaraza ya madiwani nchini, kuweka utaratibu wa kujadili masuala yanayowahusu watu wenye ulemavu kwenye vikao vyao ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Alisema hayo juzi wakati wa kuapishwa kwa madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Nderiananga alisema ni vizuri halmashauri zianze kuangalia kundi la watu wenye ulemavu na kuweka mipango ya kuwasaidia ili waendelee kutoa mchango wao katika kukuza uchumi wa nchi.

Alisema kama vikao muhimu vinaweza kujadili mambo ya wanawake, vijana na wazee, kuna tatizo gani kujadili changamoto za watu wenye ulemavu na kuwashirikisha kwenye programu mbalimbali.

“Kuanzia sasa masuala ya watu wenye ulemavu yajadiliwe kwenye vikao maalumu na kutolewa uamuzi , sisi kama Wizara tutaendelea kutoa maagizo kwa nchi nzima, ikiwa ni utekeleza wa ilani ya CCM na maono ya Rais John Magufuli,” alisema .

Aidha aliwataka wanapojenga majengo wahakikishe wanaweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Mbunge wa Viti maalum Esther Maleko(CCM) aliwaomba madiwani wafanyekazi kwa ushirikiano kuleta maendeleo kwa sababu wananchi wanawategemea.

Katika kikao cha baraza hilo, madiwani walimchagua diwani wa kata ya Okaoni, Moris Makoi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kura 46 na Makamu Mwenyekiti ni Filberth Shayo aliyepata kura 47.

Join our Newsletter