Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 14Article 518471

Siasa of Monday, 14 December 2020

Chanzo: HabariLeo

Madiwani waomba msamaha kwa kuchafua viongozi WhatsApp

Madiwani waomba msamaha kwa kuchafua viongozi WhatsApp

WIKI moja tu baada ya kula kiapo cha kuwatumikia wananchi, madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wamekuwa wa kwanza kukiri kuwa sehemu ya mifarakano na uchochezi ndani ya chama chao Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kutokana na ukweli huo, madiwani hao wamekiomba msamaha chama hicho, viongozi wake na umma kwa ujumla.

Hatua hiyo imekuja baada ya hivi karibuni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ya CCM (MNEC), Salim Asas kuwatuhumu baadhi ya wana CCM kutumia makundi katika mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp, kushirikiana na baadhi ya wapinzani kuwatukana baadhi ya viongozi wa chama na serikali yao.

Akiomba radhi kwa niaba ya madiwani hao mbele ya MNEC huyo juzi, Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada alisema; “wenzangu wamenituma kwa niaba yetu wote, tukuombe radhi wewe binafsi, chama chetu na watanzania kwa sababu katika mchakato wetu wa uchaguzi, sisi tulikuwa sehemu ya makundi yanayochafua viongozi wetu, ukiwemo wewe.”

Aliomba msamaha huo juzi mjini Iringa wakati madiwani wote wa halmashauri hiyo waliochaguliwa kupitia CCM, walipokuwa kwenye mafunzo ya majukumu yao kwa wananchi, maadili na maslahi ya chama chao katika kuwaongoza wananchi.

“Kama umetukanwa wewe na baadhi ya viongozi wengine ni kwa sababu ya sisi madiwani; tumekudhalilisha sana na tumewatuma baadhi ya watu mitandaoni wawatukane na kuwakashifu huku sisi tukisheherekea upuuzi huo,” alisema bila kuwataja madiwani waliokuwa wakifanya vitendo hivyo mitandaoni.

Meya alisema matendo ya madiwani hao, yamewajeruhi viongozi hao na familia zao, biashara zao na shughuli zao zingine katika jamii kwa sababu mengi wanayoyafanya ni ya uzushi na uongo, yakichochewa na ubinafsi.

Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Said Rubeya alisema

“Tunajua maumivu unayopata katika ushiriki wako wa kujenga chama hiki na kuchangia maendeleo ya watu wa Iringa. Maumivu hayo yanasababishwa na watu unaowasaidia pia, ambao hawapendi kuona ukisaidia shughuli zingine na kwa kushirikiana na wapinzani wetu kisiasa wanakupiga vita.”

Kwa niaba ya CCM Manispaa ya Iringa, Rubeya alisema ameupokea msamaha wa madiwani hao na aliahidi kuufikisha katika vikao vya chama kwa kumbukumbu za chama hicho.

Akipokea ombi la msamaha wa madiwani hao wakati akifunga mafunzo hayo, Asas alisema; “Ni jambo la kawaida kwa viongozi kusemwa, lakini wanaposemwa kwa kuzushiwa uongo na kwa kupitia nje ya taratibu za Chama hakuna afya zaidi ya kuchochea mgawanyiko na uadui.”

Aliwataka wanaCCM kuwa makini na wasiendelee kuteleza kwa kuwatumia wasio wana CCM kupenyeza mambo yao yasiyo na afya kwa chama hicho kikubwa.

Alisema ni kawaida kwa chama kikubwa kama chao kupitia mifarakano wakati wa michakato ya uchaguzi, lakini ni utamaduni wao baada ya shughuli hizo, wana CCM kuwa wamoja na kuwasaidia viongozi kusimamia utekelezaji wa Ilani na ahadi zao.

Asas alisema baada ya uchaguzi mkuu kwisha, wana CCM kwa ujumla wao wana ajenda moja tu ya kuwatumikia wananchi huku wakidumisha umoja na mshikamano ili kufanikisha majukumu yaliyopo mbele yao.

“Kwa kuwa mmeomba msamaha, lugha yetu iwe ni umoja na mshikamano. Mbele yako meya, mwenyekiti wa CCM wa Manispaa yetu na madiwani wa kata zote 18 niseme niko tayari kushirikiana na madiwani wote kusukuma gurudumu la maendeleo ya mji wetu,” alisema.

Katika kuboresha utendaji wa madiwani wa halmashauri hiyo, Asas alisema ameombwa na tayari ameanza kukarabati ofisi ya meya na ya mbunge wa jimbo la Iringa Mjini zilizokuwa ndogo.

Alisema ombi la kukarabati ofisi hizo, lilitolewa na mbunge wa jimbo hilo, Dk Jesca Msambatavangu na halmashauri ya manispaa hiyo iliyokiri kwa sasa kutokuwa na fedha za kufanya ukarabati mkubwa wa ofisi hizo.

Pamoja na kukarabati ofisi hizo, Asas aliahidi pia kuyashughulikia matatizo mbalimbali katika jimbo hilo yanayohitaji mchango wa wananchi kufanyiwa kazi kwa haraka, ikiwa ni pamoja na upungufu wa madawati katika baadhi ya shule za mji huo.

Katika ndoto zake, Asas alisema anataka baraza hilo la madiwani liweke historia kwa kukumbukwa katika kipindi cha miaka 50 ijayo, kwa kufanya mambo yatakayoibadilisha halmashauri hiyo na wananchi wake kimaendeleo.

Join our Newsletter