Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 05Article 513922

xxxxxxxxxxx of Thursday, 5 November 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Majimbo yampa kura za kishindo

USHINDI wa Rais Mteule, Dk John Magufuli umedhihirisha imani waliyokuwa nayo Watanzania kwake na kwa chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Udhihirisho huo unaelezwa ulibebwa na matokeo chanya ya yale aliyofanya Dk Magufuli kwa miaka mitano ya kipindi cha kwanza cha uongozi wake wa Awamu ya Tano.

Katika uchaguzi huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Dk Magufuli kuwa mshindi kwa kupata kura 12,516,252 kati ya kura halali 14,830,195 zilizopigwa na wapigakura.

Wingi huu wa kura tayari umemfanya Rais mteule Magufuli kusema kuwa ana deni kubwa kwa Watanzania kutokana na imani waliomuonesha kupitia kura hizo. Dk Magufuli pia amewataka viongozi wenzake wakiwamo wabunge wateule na madiwani wateule kwamba wana wajibu mkubwa wa kufanya kwa Watanzania.

Mambo hayo ni pamoja na miradi mikubwa iliyofanyika ikiwamo Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), vituo vya afya, elimu bure, barabara, madaraja ya juu na ya kawaida, umeme vijiji zaidi ya 9,000 na mengine mengi ambayo hesabu yake inaelezwa ilitolewa na Watanzania katika masanduku ya kura Oktoba 28, mwaka huu.

Kwa mujibu wa matokeo ya baadhi ya majimbo katika mikoa ambayo gazeti hili lilifanikiwa kuyanukuu yaliyokuwa yakitangazwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, Oktoba 29 na 30 mwaka huu, yanaonesha kuwa Magufuli amepata ushindi wa kishindo katika maeneo hayo.

Kwa mfano, katika Mkoa wa Tanga, kwa majimbo machache ambayo gazeti hili ilirekodi matokeo yake, Dk Magufuli alipata kura 386,871. Aidha, kwa baadhi ya majimbo ya Mkoa wa Kagera, Magufuli alipata kura 473,578, Singida kura 234,255, Mtwara kura 283,999 na Tabora kura 226,249.

Kwa baadhi ya majimbo ya mikoa mingine ikiwamo Mkoa wa Manyara, Magufuli alipata kura 228,759, Mjini Magharibi kura 143,169, Mbeya kura 238,821, Kaskazini Pemba kura 15,678, Iringa kura 197,367 na Kusini Unguja kura 46,731.

Maeneo mengine ambayo gazeti hili lilirekodi matokeo yake kwa baadhi ya majimbo ni Mkoa wa Simiyu ambako Magufuli alipata kura 352,222, Mara kura 339,447, Kilimanjaro kura 184,007, Kaskazini Unguja kura 40,764 na mkoani Njombe kura 189,300.

Imani hiyo ya wananchi kwa Magufuli pia imedhihirika katika Mkoa wa Dar es Salaam ambako alipata kura 1,503,317, Kigoma kura 229,217, Katavi kura 159,591, Rukwa kura 144,298, Geita kura 123,054, Ruvuma kura 248,158, Shinyanga kura 300,186, Pwani kura 295,920 na Arusha kura 358,638.

Ushindi huo wa kishindo kwa Rais Magufuli pia ulidhihirishwa na wananchi wa Mkoa wa Mwanza ambako Magufuli kwa majimbo kadhaa alipata kura 944,467, Songwe kura 155,791, Morogoro kura 779,672, Lindi kura 193,224 na Dodoma kwa majimbo machache alipata kura 421,666.

Katika Mkoa wa Kusini Pemba, Magufuli alipata kura 6,047 kwa baadhi ya majimbo.

Kwa ujumla, Dk Magufuli amepewa kura nyingi na Watanzania katika mikoa yote nchini, ikidhihirisha kuwa wamevutiwa na jinsi serikali yake katika muhula wake wa kwanza ilivyowatumikia wananchi wake kwa mafanikio makubwa. Inatarajiwa baada ya NEC kukamilisha hesabu zake, tutajua wapi amepata kura nyingi zaidi.

Leo Rais Magufuli anatarajiwa kuapishwa, kisha taifa litakuwa na hamu ya kusikia baraza jipya la mawaziri litakalomsaidia kusimamia wizara atakazounda au watakaosimamia zilizopo kama hatafanya mabadiliko yoyote.

Utendaji kazi wake umehitimishwa kwa ushindi huu wa kihistoria ambao kwa sasa ahadi alizotoa wakati wa kampeni zinasubiriwa kuanza utekelezaji wake na mwendelezo wa miradi iliyokwisha anza baada ya baraza hilo la mawaziri.

Mapema wiki hii, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi alinukuliwa akisema Watanzania wamechagua mwendelezo wa mageuzi na si blabla zisizo na mashiko.

Dk Abbasi anasema kazi kubwa zenye matokeo chanya alizofanya Rais Magufuli kipindi cha kwanza cha uongozi wake, ndio hasa kinachobeba ushindi wa kishindo alioupata, hivyo alistahili ushindi huo.

Anasema watendaji watakaofanikiwa kufanya kazi na Dk Magufuli katika kipindi cha pili cha awamu hii ya tano, wanapaswa kutambua kuwa ushindi na deni analosema Magufuli analo kwa Watanzania, si lake peke yake, bali ni la watendaji wanaotarajiwa kutekeleza wajibu wao kumsaidia Rais kufikia malengo na ahadi alizotoa.

Anasema kama kuna aliyebweteka akijua hiki ni kipindi cha lala salama, anajidanganya kwani ndio hasa kipindi cha udhihirisho mwingine wa mageuzi makubwa yanayoendelea kutekelezwa na Serikali ya CCM kupitia Rais Magufuli.

Makala hii imeandikwa na Halima Mlacha, Gloria Tesha na Matern Kayera

Join our Newsletter