Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 28Article 516410

Siasa of Saturday, 28 November 2020

Chanzo: HabariLeo

Makamu Mwenyekiti ampiku mwenyekiti kura za maoni

Makamu Mwenyekiti ampiku mwenyekiti kura za maoni

ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Babati Vijijini, John Noya amemwangusha aliyekuwa mwenyekiti wake katika kipindi cha 2015 hadi 2020 kwa kupata kura 23 dhidi ya kura 12 za mtangulizi wake Nicodemas Tarimo katika kura za ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkutano huo wa uchaguzi ndani ya CCM pia ulimpitisha Yahaya Loya kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura 22 dhidi ya Filbert Fransis aliyepata kura tisa huku mgombea wa tatu Sabin Sarme akipata kura 3 hakuna kura zilizoharibika.

Katika mkutano huo kulikuwa na wajumbe wapigakura 35 kati yao akiwepo Mbunge wa Jimbo hilo Daniel Sulle.

Baada ya ushindi huo kutangazwa, John Noya alijielezea kuwa ana uzoefu wa kutosha katika nafasi hiyo, kwani amekaa kwa miaka mitano kama makamu na kujifunza yote yanayohusu nafasi hiyo ya uenyekiti wa halmashauri kwa kuendesha na kuongoza vikao vya mabaraza yao.

Katibu wa CCM wilaya ya Babati Vijijni, Filbert Mampwepwe aliwataka madiwani wapongezane kwa sababu uchaguzi umeisha salama.

Pia aliwataka Madiwani waache utoro wa kutoshiriki vikao vya chama na kuishia kushiriki vikao vya Baraza la madiwani vyenye posho kubwa.

“Kwa kuwa tumevunja makambi baada ya kumaliza uchaguzi hivyo sitegemei kuona kura ya (hapana) kwenye uchaguzi utakaosimamiwa na serikali za mitaa,” alionya Mampwepwe.

Join our Newsletter