Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 07Article 517601

xxxxxxxxxxx of Monday, 7 December 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Mbunge Chadema kufikisha bungeni sakata la askari Tawa

MBUNGE wa Jimbo la Nkasi Kaskazini mkoani Rukwa, Aida Khenan amesema atafikisha katika Bunge la 12 sakata la askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), wanaodaiwa kuteketeza nyumba 150 zinazodaiwa kuwa zimejengwa ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Akiba wa Lwafi.

Alisema hayo alipohojiwa na HabariLEO kuhusu tukio hilo. Alieleza kuwa askari wa Tawa wapatao 15 waliteketeza kwa moto nyumba hizo Novemba 5 mwaka huu. Siku hiyo Rais John Magufuli na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan walikuwa wakiapishwa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Mbunge huyo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)alihudhuria sherehe hiyo.

Alisema nyumba hizo zilizoteketezwa kwa moto ni za wakazi wa Kata ya Itete iliyopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika Wilaya ya Nkasi.

"Mkasa huu wa wakazi wa Kata ya Itete kuchomewa nyumba nilimweleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa nilipokuwa bungeni... Nyumba zingine zimeezekwa kwa bati, sasa wanawake wengine wajawazito na watoto wachanga wanalala nje, wamechomewa nyumba waende wapi, nilimjulisha mkuu wa mkoa Rukwa na mkuu wa wilaya Nkasi lakini nao hawakuwa na taarifa hiyo”alisema na kuongeza:

“Idadi ya nyumba zilizoteketezwa kwa moto taarifa zinakinzana, ipo taarifa ya nyumba 150 na nyingine nyumba 200 hadi 300'' alisema.

Alieleza mipaka inayotenganisha kata ya Itete na hifadhi, bado ni changamoto kubwa. Aliomba serikali iandae ramani mpya ili kuepusha mgogoro, kwa kuwa watu hao wameishi katika eneo hilo zaidi ya miaka saba.

Aliwataka wananchi wanaoishi jirani na mapori tengefu ya hifadhi, wasivunje sheria kwa kukata miti na kuchoma mkaa. Alisisitiza kuwa hakuna haki bila wajibu na serikali wajibu wake ni kupima upya mipaka inayogombaniwa na pande hizo mbili.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda aliwataka madiwani kuwasilisha hoja katika baraza lao kuomba kipande cha ardhi kimegwe kutoka Hifadhi ya Misitu ya Akiba Lwafi na wakabidhiwe wananchi walime.

Alimuomba Khenan kuwasilisha hoja hiyo katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na kuiwasilisha serikalini ili wananchi wapate ardhi kwa ajili ya kilimo.

Mtanda alitoa maagizo hayo baada ya kusomewa taarifa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Itete, Robert Matwiga kwamba askari wa Tawa waliteketeza kwa moto nyumba 150, kwamba ziko hifadhini.

Mtanda alifika Itete akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama wilaya.

"Hoja hii ikipita katika baraza la madiwani mie kama DC nitaandika barua maalumu kusisitiza muhimu wa wananchi kutengewa kipande cha ardhi hifadhini ili wapate eneo la kulima,"alisisitiza.

Aliwataka Tawa kuweka mipaka ya kudumu kwa kuchimbia mawe makubwa ardhi yakiwa na maandishi, badala ya kusimika vibao ambavyo ni rahisi kuhamishika.

Alikiri kuwa eneo la ardhi wanaloishi wakazi wa kijiji cha Itete ni dogo. Alisema idadi ya wakazi hao inaongezeka lakini ukubwa wa ardhi hauongezeki.

Mtanda alimwagiza Ofisa Ardhi Wilaya ya Nkasi, kupima upya eneo hilo la mpaka kwa GPS, akimpatia siku saba awe amekamilisha ripoti yake ili ukweli ubainike.

Join our Newsletter