Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2021 01 09Article 520847

Siasa of Saturday, 9 January 2021

Chanzo: HabariLeo

Mbunge Tanga akabidhi mifuko 600 saruji ujenzi wa madarasa

Mbunge Tanga akabidhi mifuko 600 saruji ujenzi wa madarasa

WAZIRI Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu amekabidhi mifuko 600 ya saruji yenye thamani ya Sh milioni 8.4 kwa ajili ya kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari jijini Tanga

Hafla ya makabidhiano ilifanyika jana mbele ya Mstahiki Meya wa Jiji hilo Abdulrahman Shiloo, Mkurugenzi Mtendaji, Daudi Mayeji pamoja na watendaji mbalimbali wa Halmashauri hiyo.

Alisema wakati wa ziara yake hivi karibuni aliahidi kupeleka mifuko ya saruji katika shule tano kati ya kumi ambazo zinaendelea na ujenzi ili kuongeza kasi ya ujenzi ili ifikapo Januari 11 wanafunzi wote waliofaulu waweze kuanza kidato cha kwanza.

"Nimevutika na jitihada ambazo Tanga Jiji mmeweza kuzifanya za kuusimamia ujenzi wa madarasa kwa nguvu kubwa hivyo nimeona niwaunge mkono ili muweze kukamilisha kwa wakati na wanafunzi wetu waweze kuanza masomo katika muda muafaka" alisema Waziri Ummy.

Hata hivyo aliwataka wakuu wa shule na kamati za zake kuzingatia miongozo ya serikali katika kuwachangisha fedha wazazi kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya elimu ya vijana wao ili kusiwepo na malalamiko wala manunguniko.

"Niwaombe endapo kuna ulazima wa kuchangisha wazazi kwa ajili ya wanafunzi hao ni lazima suala hilo kujadiliwa na kukubaliwa na Wazazi/Walezi wenye watoto katika shule husika badala ya kamati kujiamulia wenyewe" alishauri Waziri Ummy.

Aidha Mstahiki Meya Shiloo alisema msaada huo umekuja wakati muafaka wanapofanya jitihada za kumaliza madarasa 44 ili wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza wanaoanza.

Hata hivyo Mkurugenzi Mayeji alimshukuru Waziri Ummy akisema kwa muda mrefu walikosa hamasa ya mtu ambaye anajitoa kwa ajili ya kuhakikisha maendeleo ya Jiji hilo katika sekta mbalimbali.

"Hii kasi uliyokuja nayo Mheshimiwa Mbunge tulikuwa tumeimiss (tumeikosa) sana, hivyo tutakualika wakati mwingine uje kuona namna tunavyotekekeza zoezi la utengenezaji wa viti na meza kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza" alisema Mayeji.

Join our Newsletter