Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 29Article 516530

xxxxxxxxxxx of Sunday, 29 November 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Mbunge ajitosa ufadhili wanafunzi 10 Veta

MBUNGE wa Makete Festo Sanga ameahidi ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 10 kila mwaka katika Chuo cha Ufundi (VETA) kilichopo Wilaya ya Makete, kwa lengo maalumu la kuwahamasisha vijana wa wilaya hiyo kukitumia chuo hicho kupata ujuzi.

Hatua ya Mbunge huyo imetokana na kutoridhishwa na idadi ndogo ya wahitimu wa Chuo hicho wanaotokea Wilaya hiyo ikilinganishwa na wahitimu wanaosoma chuoni hapo kutokea mikoa mbalimbali.

Akizungumza wakati wa mahafali ya sita ya Chuo hicho alisema siyo jambo la kufurahisha hata kidogo kuona kuna idadi ndogo ya vijana wa Makete wanaosoma chuo hicho ambacho kipo ndani ya wilaya yao na hivyo kuamua kuchukua juhudi za makusudi kuhakikisha idadi ya wanafunzi hao inaongezeka.

"Inasikitisha kuona kati ya wanafunzi 64 wanaohitimu leo, wanafunzi wanaotokea hapa Makete hawafiki 10, zaidi ya wanafunzi 50 wanatoka nje ya wilaya ya Makete, tafsiri yake ni kushindwa kutumia fursa ya uwepo wa chuo hiki kwa ajili ya kujipatia ujuzi mbalimbali," alisema Sanga

Alisema katika kutoa hamasa ili vijana wa wilaya hiyo waweze kujiunga na masomo katika Chuo hicho, ataweka mpango maalumu kwa kuwagharamia masomo wanafunzi 10 wanaotokea katika mazingira magumu kila mwaka.

Alisema kama Mbunge wa Jimbo hilo, hawezi kukubali kuona uwekezaji wa Chuo hicho ambao umeigharimu serikali mabilioni ya fedha ukishindwa kuwanufahisha wana Makete kupata ujuzi, hatua ambayo ameona vyema kuingilia kati kwa lengo la kueta mabadiliko kwa wilaya hiyo na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Makete Xavier Meta alisema pamoja na mafanikio waliyoyapata tangu kuanzishwa kwa chuo hicho, bado wanakabiliwa na changamoto ikiwemo ya uchache wa vyumba vya madarasa hali inayosababisha msongamano wa wanafunzi darasani.

Alisema katika kulitatua hilo, wamejipanga kuongeza idadi ya madarasa manne ambayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza udahili zaidi sambamba na ujenzi wa maktaba utakaosaidia zaidi ufaulu mzuri kwa wanafunzi.

Kwa upande wao wanafunzi wanaomaliza chuo wameomba kuongezwa kwa kozi nyingine kama ufundi bomba, mapishi, umeme wa magari na majumbani na zingine ili kusaidia kupata watalaamu wengi lakini pia kumfanya mwanafunzi kuchagua fani anayoipenda kusomea tofauti na sasa ambapo wanalazimika kusomea fani ambazo hawajazichagua.

Join our Newsletter