Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 09 25Article 510319

Siasa of Friday, 25 September 2020

Chanzo: HabariLeo

Mgombea ubunge Chadema ataja vipaumbele 7

Mgombea ubunge Chadema ataja vipaumbele 7

MGOMBEA ubunge Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Devota Minja amesema amekusudia kumsaidia mama na mtoto kwa kujenga duka la dawa nafuu nje ya jengo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo.

Minja aliyasema hayo wakati akifanya kampeni katika Kata ya Boma iliyopo katika Manispaa ya Morogoro.

Alisema akichaguliwa kuwa mbunge wa Morogoro Mjini, vipaumbele vyake vitakuwa ni pamoja na maendeleo ya viwanda, huduma za afya, maji, kuanzisha chama cha ushirika cha kuweka na kukopa (saccos) kwa ajili ya wananchi wa manispaa, miundo mbinu na kuhakikisha wanapunguza mrundikano wa wanafunzi darasani.

Akizungumzia afya, mgombea huyo kupitia Chadema alisema amedhamiria kupitia milioni 57 za Mfuko wa Jimbo anazopewa kila Mbunge, kuanzisha duka la dawa la hati punguzo.

Alisema duka hilo litakuwa na vifaa tiba vitakavyokuwa vinapatikana kwa bei nafuu ili kila mwananchi amudu gharama za kununua.

Alisema hospitali nyingi za Serikali hazina dawa zinazotosha, hivyo duka hilo litakalotoa huduma kwa saa 24, litasaidia upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu na huduma ya uhakika.

"Kama mtu ana ndugu yake amelazwa na anahitaji huduma na kwa wakati huo akiwa hana pesa, atatakiwa kufika dukani na kujiandikisha kisha kupata huduma aitakayo na baadaye kufanya malipo baada ya kutafuta," alisema.

Devota alisema, kupitia duka hilo la hati punguzo pia utasaidia pia wajawazito wanaokosa vifaa vya kujifungulia kupata vifaa hivyo ili kupunguza vifo vya wajawazito wanaopoteza maisha kwa kukosa vifaa tiba.

"Tunataka kuhakikisha kuwa mtu hapotezi maisha kwa kukosa Sh 1,000 ya Panadol, mtu hapotezi maisha kwa kukosa hela ya kununua dripu au bomba la sindano," alisema Devota.

Alisema duka hilo litaondoa changamoto ya watoto wenye umri wa miaka mitano kupoteza maisha kwa kukosa dawa wanapougua na ndugu kutakiwa kununua hata kama hawana uwezo katika kipindi hicho.

"Najua watoto wa chini ya miaka mitano ndio wanaosumbuliwa na magonjwa kila mara na magonjwa ya mara kwa mara ni ya wajawazito, hivyo duka hilo litakuwa msaada mkubwa sana kwa makundi haya," alisema Devota.

Join our Newsletter