Uko hapa: NyumbaniHabariSiasa2021 09 11Article 556888

Siasa of Saturday, 11 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Msajili abaini Chadema kukiuka utunzaji mali

Msajili abaini Chadema kukiuka utunzaji mali Msajili abaini Chadema kukiuka utunzaji mali

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa hakizingatii uwekaji wa kumbukumbu za mali za chama chao kwa mujibu wa kanuni za fedha na usajili.

Kimetakiwa kuwa na orodha ya mali na aina za mali husika na kuhakikisha wanatumia bajeti iliyoidhinishwa na Kamati Kuu, tofauti na wanavyofanya sasa kutumia bajeti isiyoidhinishwa.

Aidha, wametakiwa pia kuweka picha ya Rais wa nchi, Samia Suluhu Hassan katika ofisi za kiongozi wa chama hicho badala ya kuweka picha ya Katibu Mkuu, John Mnyika.

Ndani ya ofisi hizo ukutani imewekwa picha ya Mnyika na mezani kukiwa na Bendera ya Taifa.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa uhakiki katika chama hicho, Msajili Msaidizi, Sixty Nyahoza alikitaka chama hicho kuwa na mipango ya manunuzi ya chama.

Aidha, aliwataka kutoingia kudhamini mikopo ya wanachama hususani viongozi wa chama hicho na waingize mikopo benki kuhakikisha kuna urejeshwaji.

Alitoa kauli hiyo kutokana na kuwepo taarifa za aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji kupewa mkopo, lakini akihama kwenda chama kingine ambacho ni Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kama mna mtendaji ambaye sio muajiriwa katika chama chenu msiingie kwenye udhamini kwa kuwa linawaletea tatizo kwa chama kwani ni lazima kuwe na urejeshwaji,” alisema Nyahoza na kupongeza mfumo wa kidigitali wa chama hicho wenye orodha ya wanachama wote.

Kuhusu ajira kwa watendaji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalim alisema katika chama hicho hakuna mwenye mkataba wa ajira, bali wanajitolea kuanzia Juni 2020.

Alipongeza uhakiki unaofanywa na Ofisi ya Msajili, na kwa yale mapungufu machache yaliyoainishwa, alisema wameyapokea na kuahidi kuyafanyia kazi.