Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 16Article 518663

Siasa of Wednesday, 16 December 2020

Chanzo: HabariLeo

Mtemvu akerwa na ubovu wa madaraja

Mtemvu akerwa na ubovu wa madaraja

MBUNGE wa Kibamba, Issa Mtemvu amekerwa na utekelezaji mbovu wa ujenzi wa miundombinu hususani madaraja na vivuko yasiyokidhi viwango.

Hayo yamebainika katika ziara yake kwa wananchi wa jimbo hilo, iliyolenga kuwashukuru kwa kumchagua na kuainisha mipango yake ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kuna haja ya kufuatilia zabuni na kandarasi za ujenzi wa miundombinu katika jimbo la Kibamba ili kubaini wanaopewa kama wana sifa au la.

“Nimeshuhudia madaraja na vivuko ambavyo havipitiki licha ya kuwa ujenzi wake hauna muda mrefu, suala linaloonesha kuwa kuna shida,” alisema Mtemvu.

Alisema atafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha thamani ya pesa inayowekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu hiyo, inaendana na ubora wa kazi husika.

Aliwataka watendaji wa serikali na viongozi wa chama jimboni mwake, kutekeleza wajibu wao ili kuzitendea haki nafasi walizonazo katika kuhakikisha thamani ya pesa inaendana na ubora wa kazi au miundombinu inayojengwa.

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Ubungo, Pili Mustafa aliwashukuru wanachama wa CCM Kata ya Kibamba hususani akina mama na vijana kwa kujitokeza kwa wingi wakati wa upigaji kura, ambao umeleta matunda mazuri ya ushindi kwa CCM.

“Niwashukuru akina mama, vijana na wote mlioshiriki katika kuichagua CCM kwa kumpigia kura diwani, mbunge na Rais”, alisema Pili.

Alisema kazi iliyobaki ni kuwasaidia viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao, ambayo ni kutoa taarifa za kero zilizopo ili wasaidie katika kupata ufumbuzi na hatimaye maendeleo ya jimbo na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ubungo, Lucas Mgonja alimpongeza mbunge wa jimbo hilo kwa kukukumbuka kurudi na kuwashukuru wananchi, kitu ambacho kinatoa matumaini kwao kwa kiongozi wao yupo na anawakumbuka.

Alisema wapo viongozi wachache ambao hukumbuka kuwashukuru wananchi. Hivyo, alimtaka mbunge huyo kuendeleza utamaduni huo kwa kuwa ni njia ya kupata mrejesho wa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hivyo kuweza kuwasemea bungeni kwa ushahidi.

Join our Newsletter