Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 16Article 518894

Siasa of Wednesday, 16 December 2020

Chanzo: HabariLeo

Ndugai asema hakuna sababu ya kukimbia nchi

Ndugai asema hakuna sababu ya kukimbia nchi

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amewaapisha wabunge wanne wa Chama cha ACT Wazalendo na kusisitiza kuwa hakuna sababu ya kukimbia nchi.

Nao wabunge waliopa jana, wamemhakikisha Spika kuwa hawatakimbia nchi na kwenda kushitaki mambo ya Tanzania nje ya nchi.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wabunge hao, Ndugai alisema:“wanao jaribu kukimbia nchi, itoshe kusema kila la heri maana kuna baridi huko, unakimbia nyumbani kwenye joto zuri na hasa mwezi huu wa Desemba. Hakuna sababu ya kukimbia nchi, nchi yetu ni nzuri na tunachohitaji ni amani, umoja, ushirikiano na mshikamano”.

Alisema kwa sasa Bunge lina wabunge wa kutosha na wamefikisha akidi ya Bunge kufanya maamuzi ya kibunge.

“ Niwahakikishia tutalinda haki zenu na ni wajibu wa Spika kuhakikisha wabunge walio wachache wanapata haki ya kusikilizwa” alisema.

Aidha, Ndugai alisema pamoja na wabunge hao kuchelewa, hakuna kanuni waiyovunja na wako katika utaratibu wa kanuni.

Walioapishwa jana ni Mbunge wa Wete, Omary Ali Omari, Mbunge wa Mtambwe, Khalifani Mohamed Issa, Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji na mbunge wa Chonga, Salum Mohamed Shafi.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge hao, Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji alisema hatua ya wao kuchelewa kuapa, isichukuliwe kwamba walikuwa wanakwepa majukumu yao.

Alisema baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu, chama chao kililazimika kutumia muda kupitia maoni ya wananchama wao, kukaa vikao vya kichama na kujiridhisha hatua kwa hatua kila jambo ambalo watalifanyia maamuzi.

“Ninayo furaha kukwambia kuwa uwepo wetu hapa una baraka ya Mwenyezi Mungu, una baraka za chama chetu na una baraka za wapigakura wetu…hivyo uwepo wetu hapa umekubalika katika ngazi zetu zote, Mheshimiwa Spika usiwe na shaka na ubunge wetu” alisema.

Alisema ACT Wazalendo iko katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa na imeamua kufanya hivyo ili kuleta amani na usalama na utulivu katika visiwa vya Zanzibar.

“ Kuna maneno mengi, wakosoaji wetu wanasema mengi kuhusiana na uamuzi wa chama chetu, lakini nikuthibitishie chama chetu kina uongozi imara kuanzia tawi hadi taifa, maamuzi yaliyoamuliwa na viongozi wetu wa juu ni maamuzi ambayo yamezingatia maslahi mapana ya taifa na maslahi ya Wazanzibari na uhai wa watu wetu” alisema.

“ Kwa hiyo Mheshimiwa Spika nikuthibitishie kwamba wale wanaokebehi na wanaodharau mapatano yale muda utawajibu na wataonea aibu kauli na matendo yao.

“ Tumezoea kushuhudia chaguzi za Zanzibar zikituacha na makovu, mwelekeo wa sasa wa Rais wetu wa Zanzibar ni jambo analolifanya kila Ijumaa kwenda misikiti mbalimbali akihubiri amani ; na maridhiano ya kweli ni ushahidi kwamba anakabidhi Mwenyezi Mungu marithiano yale.

“ Pia kwa Makamu wa Rais naye kwenda katika nyumba za ibada kila ijumaa akihubiri neno la amani, neno la maridhiano ni mambo ambayo kila mtanzania anapaswa kuyaunga mkono”

“ Hatutarajii kama kuna Watanzania bado wanadharau hatua hii njema. Mheshimiwa Spika, Zanzibar ni visiwa vyetu na ni ya Watanzania wote. Tumeridhika na hatua zote ambazo zimechukuliwa na chama chetu katika kuleta umoja wa Zanzibar.

“ NaTanzania hii tutabanana hapa hapa na tutarekebishana hapa hapa Tanzania, hatutakwenda Ujerumani wala Canada kwenda kulalamikia mambo ya Tanzania” alisema.

Aidha, Haji alisema pamoja na kuwa kuna wabunge wachache, watahakikisha wanawakilisha wananchi ipasavyo.

“Mheshimiwa Spika, uwape salamu CCM kuwa udogo wetu wasiuchukulie poa hata kidogo, tumejipanga kuwawakilisha wananchi kwenye mambo yatakayowaletea maendeleo kwenye nchi yetu” alisema.

Join our Newsletter