Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 28Article 516476

xxxxxxxxxxx of Saturday, 28 November 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Sanga atoa ufadhili wanafunzi 10 wa Veta

MBUNGE wa Makete Festo Sanga ameahidi ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 10 kila Mwaka katika Chuo cha Ufundi (VETA) kilichopo katika Wilaya ya Makete kwa lengo maalumu la kuwahamasisha vijana wa wilaya hiyo kikitumia chuo hicho kupata ujuzi.

Hatua hiyo ya Mbunge huyo imetokana na kitendo cha kutoridhishwa na idadi ndogo ya wahitimu wa Chuo hicho wanaotokea Wilaya hiyo ikilinganishwa na wahitimu wanaosoma chuoni hapo kutokea mikoa mbalimbali.

Akizungumza waka wa mahafali ya sita ya Chuo hicho ambapo alikuwa Mgeni rasmi, Sanga alisema siyo jambo la kufurahisha hata kidogo kuona kuna idadi ndogo ya vijana wa Makete wanaosoma chuo hicho ambacho kipo ndani ya wilaya yao na hivyo kuamua kuchukua juhudi za makusudi kuhakikisha idadi ya wanafunzi hao inaongezeka.

"inasikitisha kuona kati ya wanafunzi 64 wanaohitimu leo, wanafunzi wanaotokea hapa Makete hawafiki 10, zaidi ya wanafunzi 50 wanatoka nje ya wilaya ya Makete, tafsiri yake ni kushindwa kutumia fursa ya uwepo wa chuo hiki kwa ajili ya kujipatia ujuzi mbalimbali” alisema Sanga

Alisema katika kutoa hamasa ili vijana wa wilaya hiyo waweze kujiunga na masomo katika Chuo hicho, ataweka mpango maalumu kwa kuwagharamia masomo wanafunzi 10 wanaotokea katika mazingira magumu kila mwaka kwa lengo la kutoa hamasa kwa vijana wengine kujiunga na chuo hicho na kujipatia ujuzi mbalimbali.

Alisema yeye kama Mbunge wa Jimbo hilo, hawezi kukubali kuona uwekezaji wa Chuo hicho ambao umeigharimu Serikali mabilioni ya fedha ukishindwa kuwanufahisha wana Makete kupata ujuzi, hatua ambayo ameona vyema kuingilia kati kwa lengo la kueta mabadiliko kwa wilaya hiyo na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Makete Xavier Meta alisema pamoja na mafanikio waliyoyapata tangu kuanzishwa kwa chuo hicho, bado wanakabiliwa na changamoto baadhi ya ikiwemo ya uchache wavyumba vya madarasa hali inayosababisha msongamano wa wanafunzi darasani.

Alisema katika kulitatua hilo, wamejipanga kuongeza idadi ya madarasa manne ambayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza udahili zaidi sambamba na ujenzi wa maktaba ambao utasaidia zaidi ufaulu mzuri kwa wananfunzi.

Kwa upande wao wanafunzi wanaomaliza chuo wameomba kuongezwa kwa kozi nyingine kama ufundi bomba,mapishi,umeme wa magari na majumbani na zingine ili kusaidia kupata watalaam wengi lakini pia kumfanya wanafunzi kuchagua fani anayoipenda kusomea tofauti na sasa ambapo wanalazimika kusomea fani ambazo hawazichagua.

Join our Newsletter