Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 08Article 517709

xxxxxxxxxxx of Tuesday, 8 December 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Serikai ya Kitaifa.. Wasomi, wanasiasa wapongeza

WAKATI nguli wa siasa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad akiapishwa leo, wanasiasa, wasomi na wananchi wamepongeza uteuzi wake, wakisema utapunguza joto na chuki za kisiasa na kuunganisha Wazanzibari.

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao alisema kilichofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya kikatiba ya kuwepo kwa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Alisema Dk Mwinyi ameonesha dhamira ya dhati ya kutimiza kwa maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Zanzibar, ambapo hilo aliliweka bayana wakati alipokabidhiwa cheti cha ushindi katika Uchaguzi Mkuu na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na alipoapishwa kushika wadhifa huo kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja.

Mwenyekiti wa Ada Tadea, Juma Ali Khatib alimpongeza Dk Mwinyi kwa kuonesha moyo wa dhati wa ushirikiano wa serikali yake kufanya kazi ya kuleta umoja na mshikamano kwa kuwaunganisha watu wote kuwa kitu kimoja.

Alisema ili Zanzibar ipate maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali, maelewano na kuwaunganisha watu wa pande zote mbili unahitajika kwa kiwango kikubwa.

Mkurugenzi wa Redio Swahiba FM, Nassra Nassor Suleiman alifurahishwa na uamuzi wa ACT Wazalendo kuingia katika SUK ambayo itasaidia kupunguza joto la kisiasa lililopo sasa na kuwaunganisha watu wote.

Nassra alisema nguvu ya pamoja na dira ni mshikamano ambapo hivi sasa zipo kila dalili ya Zanzibar kupata maendeleo makubwa ya kiuchumi, kijamii na kifikra.

“Matumaini yetu Maalim Seif atafanya kazi bega kwa bega kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wetu,” alisema mkurugenzi huyo.

Mkazi wa Mikunguni, Juma Almasi alisema “Wazanzibari tunataka maendeleo na sio chuki za uhasama wa kiaisa.” Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi alisema umoja wa kitaifa ni jambo zuri kwa kuwa litaleta amani na kwa njia ya amani itakuwa rahisi kwa Wazanzibari kujiletea maendeleo ya kweli.

Alisema katika nchi ambazo amani imetoweka, fursa ya kutulia na kujenga uchumi haipo hivyo Wazanzibari wanapaswa kuungwa mkono kuweka tofauti zao za kisiasa pembeni na kuamua kujenga uchumi na ustawi wa jamii.

“Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, ndiyo maana licha ya ACT Wazalendo kushindwa uchaguzi, lakini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliona kwamba licha ya wenzao kushindwa lakini wote ni Wazanzibari, waliona vyema waje pamoja, washirikiane ili Zanzibar kuwe na maendeleo,” alisema Profesa Moshi.

Mtaalamu wa Siasa ya Jamii wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Samwel Maghimbi alisema siasa ina maslahi kwa kuwa ina vitu vya kutoa na vitu vya kuchukua, ndiyo maana iliwabidi ACT Wazalendo waainishe kwanza mikakati yao kabla ya kukubali kuingia kwenye serikali ya umoja wa kitaifa.

“Ilikuwa lazima wafanye mikakati kwa kuwa jambo hili ni siasa, ilibidi wakae chini wafikirie waone kama wanapata maslahi gani, bila shaka wameona kuliko watoke kabisa kwenye ulingo wa siasa za Zanzibar, wameona uamuzi walioufanya unaweza kuwasaidia,” alisema.

Imeandikwa na Khatib Suleiman (Zanzibar) na Matern Kayera (Dar).

Join our Newsletter