Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 05Article 513892

Siasa of Thursday, 5 November 2020

Chanzo: HabariLeo

Ubunge ni utumishi wa umma, haujali chama

Ubunge ni utumishi wa umma, haujali chama

KWA matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu, inamaanisha kwamba Bunge la 12 haliwezi kuwa na tofauti kubwa na Bunge la mwaka 1965 ambalo lilihutubiwa na Mwalimu Julius Nyerere wakati taifa hili lilikuwa la chama kimoja.

Tofauti kubwa kati ya Bunge hilo la mwaka 1965 na hili la 12 ni kuwapo kwa wabunge wasiozidi 15 kutoka upinzani katika kipindi ambacho Tanzania inatekeleza demokrasia ya vyama vingi tangu kuanza kwa utaratibu huo mwaka 1995.

Wakati akihutubia Bunge mwaka 1965, Rais Julius Nyerere alizungumzia uchaguzi wa mwaka huo ambao ulikuwa wa aina yake kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania mwaka 1964. Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tanganyika na Zanzibar ilikuwa aliyeteuliwa mwaka 1962 kuwa Rais wa Tanganyika awe Rais wa Tanzania.

Katika uchaguzi huo ambao Mwalimu hakupiga kampeni, wananchi wa Tanzania walifanya uamuzi kuhusu kumkubali Nyerere kuendelea kuwa Rais wa Tanzania au kumkataa.

Katika uchaguzi huo akizungumzia nafasi yake kama Rais, alihadharisha Watanzania kwamba kwa namna yoyote nafasi ya Urais ni nyeti kwani wakati wakichagua Rais na wabunge wanaamua namna sheria wanazitaka, kiasi gani cha kodi kitawekwa kwa ajili ya huduma za umma na jamii na nani atazungumza kwa niaba ya Tanzania huko nje.

Anasema hayo ndiyo ambayo Watanzania walifikiri wakati wanadai uhuru wao, walitaka kujiamulia mambo yao wenyewe, wakipanga wanachotaka kuwa na mwelekeo wanaofaa kwa mujibu wa haja zilizopo. Hatuhitaji watu wengine kutupangia hilo.

Tulitafuta uhuru, lakini kiukweli mambo yanayohusu uhuru wetu na maamuzi yetu tunakasimisha wachache kwa niaba yetu ndio maana tunafanya uchaguzi. Tunapochagua wabunge wetu na madiwani wetu tunafanya kazi ya kuwapa wajibu ambao wanastahili kuutekeleza na mwishoni kuangalia kama wamewajibika.

Pamoja na kuwepo kwa chama kimoja wakati huo yaani TANU na ASP kwa upande wa Zanzibar, Rais Nyerere alisema wazi kwamba kazi ya wabunge ni uwakilishi. Anasema akiwa bungeni anatakiwa kuzungumza kwa niaba ya watu waliomchagua hasa kuhusu utengenezaji wa sheria mpya, zinapofanyika sheria hizi ni pamoja za uendeshaji wa serikali, mapato na matumizi ambayo yanakwenda moja kwa moja katika kodi anayostahili kutozwa mwananchi.

Lakini jambo jingine, anatakiwa kuwasilisha matatizo ya wananchi kwa serikali kwa kufanyiwa kazi. Jambo jingine ni vizuri akajiunga na wenzake kuiunga mkono serikali kama anaamini kwamba inafanya vyema. Na kuibana pale inapoonekana wazi kwamba baadhi ya matendo ya serikali yanaleta shida na haiangalii maslahi mapana ya taifa.

Aidha, kazi ya mbunge ni kuhakikisha mawazo ya serikali yanafikishwa kwa wananchi na pia kuwaeleza wananchi wake anaowawakilisha nini serikali inafanya katika taifa na pia katika eneo lake la uwakilishi na kwa nini.

Kwa Mwalimu Nyerere, kitendo cha kuwa na wawakilishi kuna maana kubwa katika uendeshaji wa nchi na hasa maeneo ya uwakilishi kwa kuwa wajibu mkubwa wa kwanza wa wabunge sio kuibana serikali, bali kuhakikisha maslahi ya jimbo lake yanafanyiwa kazi kwanza.

Kauli ya Mwalimu Nyerere kwenye Bunge la chama kimoja, mwaka huo akielezea wajibu mkubwa wa wabunge katika kuimarisha maendeleo katika maeneo yao inajitanabaisha na sasa ambapo wawakilishi hawa wana kazi kubwa ya kuifanya kuhakikisha msukumo wa maendeleo kutoka katika maeneo yao ya uwakilishi unakuwa mkubwa zaidi.

Mwalimu Nyerere katika hotuba yake alisisitiza hadhi ya mwakilishi wa wananchi na kutakiwa kujiheshimu kwa manufaa ya jimbo na pia taifa. Mtu huyu anatakiwa kulijenga jimbo lake na kulijenga taifa kwa wakati huo huo.

“Ni lazima kwa mbunge kuhakikisha kwamba anaweza kujieleza mbele ya wananchi na mbele ya serikali ili kuweza kuunganisha juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla na kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere hilo linawezekana kwa mbunge kulijua tatizo la eneo lake na tatizo la taifa kwa kipindi hicho na kusaidia kutatua matatizo hayo, vinginevyo hatakuwa wa msaada kwa wananchi waliomchagua, kwa serikali na kwa taifa.

Kitu alichosisitiza Rais Nyerere wakati huo ni matokeo ya uchaguzi na kusema ni vyema yakaheshimika na watu wakaingia kazini na kuendelea kujenga nchi. Mwalimu Nyerere alisema yeye haoni sababu ya uhasama baada ya kumalizika kwa uchaguzi, maisha yanaendelea.

Jambo jingine kutokana na wingi wa wabunge wa CCM ni vyema kama wabunge hao wakatambua dhamana yao kubwa kwa taifa hili katika umoja wake.

Katika hotuba yake ya kufungua Bunge jipya Oktoba 12,1965, Mwalimu Nyerere alisema walioshindwa katika uchaguzi wasijisikie aibu kwani ilikuwa lazima ushindi uwe wa mtu mmoja, kwani kazi kubwa iliyofanyika ni kuheshimu demokrasia kwa kufanya uchaguzi.

Katika hotuba hiyo, pia alielezea historia ya mwenendo wa kura kwa mwaka 1958 na 1959 iliyosababisha matokeo kuvuta watu wengi zaidi kujiunga na TANU na kupigia kura katika miaka ya 1960 wakiangusha vigogo wengine.

Katika uchaguzi wa kwanza watu, 24,000 walishiriki lakini uchaguzi wa mwaka 1962 walijiandikisha watu milioni 1.8, lakini asilimia 64 tu walishiriki kwani watu milioni 1.2 ndio walipiga kura.

Kiukweli kama wabunge watawajibika katika majimbo yao wataifanya serikali itekeleze wajibu wake na wananchi nao kutekeleza yanayowahusu. Kwani watakuwa daraja kwa serikali na wananchi na pia kwa kuibana serikali wataifanya nchi izidi kusonga mbele.

Join our Newsletter