Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 14Article 514765

Siasa of Saturday, 14 November 2020

Chanzo: HabariLeo

Wabunge: Tanzania mpya inayong’ara inakuja

Wabunge: Tanzania mpya inayong’ara inakuja

WABUNGE wamesema kutokana na maono, dira na vipaumbele alivyoainisha Rais John Magufuli vya kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo, wanaiona kesho mpya inayong'ara na Tanzania yenye matumaini mapya.

Miongoni mwa waliozungumza katika mahojiano na gazeti hili baada ya Rais John Magufuli kuzindua Bunge la 12 jana jijini Dodoma, ni Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde aliyesema mkakati wa rais wa kuendelea kujenga uchumi unatoa matumaini makubwa kwa maendeleo ya Watanzania.

Mbunge wa Viti Maalumu, Jenejelly Ntate alisema amefurahishwa na hotuba ya rais kuwakumbuka wafanyakazi.

“Naiona kesho nzuri ya watumishi inayong'ara inakuja, kwani itaongeza mishahara na watakuwa na maisha bora,” alisema Ntate.

Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengelwa alisema mkakati wa Rais Magufuli wa kujenga barabara kuunganisha mikoa na wilaya kutaisaidia wakulima wa wilaya kongwe ya Rufiji kufikisha mazao yao katika masoko kwa urahisi.

Mbunge wa Makete, Festo Sanga alisema mkakati wa kujenga viwanda katika kila mkoa, unaiweka Makete kwenye ramani ya kuanzisha viwanda vya matunda, mbao na mianzi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi alisema wazo la kurasimisha tiba asilia au mbadala kunawapa nafasi waganga wa tiba asilia kutumia fursa hiyo mkoani Shinyanga kurasimisha huduma zao.

Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mayenga alisema hotuba ya Rais imemfurahisha kutokana na uamuzi wake wa kuhamisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu hadi ofisi yake (Rais) kuwajibisha watendaji waliokuwa wakikwamisha hivyo sekta binafsi itapata fursa ya kuingia katika uwekezaji.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema hotuba hiyo ni dira ya kufungua milango kwa ajili ya fursa ya uwekezaji.

Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbasi alisema hotuba inaonesha namna Tanzania itakavyopaishwa kiuchumi katika miaka mitano, wakati Mbunge wa Tunduma, David Silinde alisema Rais amegusa eneo muhimu la kufungua biashara. Alisema anaamini Tunduma litakuwa lango la biashara kwa nchi jirani.

Mbunge wa Lulindi, Issa Mchungahela alisema hotuba hiyo ni kioo kwa Watanzania kwani haijabagua, Rais amejipambanua kwamba ni mtu mwenye maono makubwa.

Katibu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi, alisema akiwa Msemaji wa Serikali, atahakikisha kila hatua iliyofikiwa na serikali inawekwa wazi. Alisema mkakati wake ni kuboresha mfumo wa utoaji taarifa za serikali ili kuwa wa kisasa zaidi katika kuwafikishia taarifa wananchi.

Join our Newsletter