Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 01Article 513499

xxxxxxxxxxx of Sunday, 1 November 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Wagombea 9 urais wakiri JPM  kashinda kihalali

WAGOMBEA urais tisa kati ya 14 walioshiriki uchaguzi mkuu mwaka huu, wamempongeza Rais Mteule John Magufuli kwa ushindi wa kishindo, aliopata na kuahidi kwa umoja kuumuunga mkono katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

Katika mkutano wao uliofanyika jijini hapa jana, kwa nyakati tofauti, walisema uchaguzi umekwisha na mshindi amepatikana kwa kupata asilimia 84.4, hivyo kilichobaki kwao na wanachama ni kushirikiana naye katika kuijenga nchi.

Walioshiriki mkutano huo na vyama vyao kwenye mabano ni Khalfan Mazrui (UMD), Queen Sendiga (ADC), Twalib Kadege (UPDP), Philip Fumbo (DP), Yeremia Maganja (NCCR Mageuzi), Cesilia Mwanga (Demokrasia Makini), Muttamwega Mgaywa (SAU), Leopard Mahona wa NRA na Seif Maalim Seif wa Chama cha Wakulima (AAFP) .

Wagombea ambao hawakushiriki mkutano huo ni Tundu Lissu wa Chadema, Bernard Membe wa ACT-Wazalendo, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, John Shibuda wa Ada-Tadea na Hashim Rungwe wa CHAUMA.

Mwenyekiti wa wagombea urais hao, mgombea urais kwa tiketi ya AAFP, Seif alimpongeza Magufuli kwa ushindi. Alisema baada ya uchaguzi kumalizika, kilichobaki ni kushikamana, kupendana na kushirikiana katika kujenga nchi ili kuendelea kujenga taifa.

"Mshindi amepatikana kwa amani na sisi kama viongozi wa vyama vya upinzani wameridhika na matokeo ya uchaguzi huo kwani umefanyika kwa uwazi, haki na usawa," alisema.

Seif alisema wanaahidi kutoa ushirikiano kwa Magufuli na wanaunga mkono juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi.

Mgombea wa Demokrasia Makini, Mwanga watamuunga mkono kutokana na ushindi aliopata kwa kishindo. Wapo tayari kumuunga mkono na kufanya naye kazi, katika kuipeleka nchi mbele kutoka katika uchumi wa kati hadi kufikia uchumi wa juu.

"Sote tumekubali kwamba Rais Mafuguli ameshinda kuwa rais na tupo tayari kufanya naye kazi bega kwa bega ," alisema.

Mgombea wa DP, Fumbo alisema nafasi ya urais ni moja hivyo wasingeweza wote kushinda wagombea wote 15. Alisema Magufuli amestahili kushinda kwa kura nyingi, kwani mchakato ulikuwa wa wazi. Alisema hakuna haja ya kugombea fito kwani wanajenga Tanzania moja.

Aliwataka Watanzania kutunza amani iliyopo nchini, akisisitiza kwamba hakuna nchi nyingine ya kukimbilia kama zikitokea vurugu.

Kadege wa UPDP alisema uchaguzi umefanyika kwa njia halali, hakukuwa na vikwazo, kificho wala figisu. Alisema uchaguzi ni demokrasia hivyo ni lazima mmoja ashinde.

Alisema kutokana na Watanzania kuridhika na utendaji wake wameamua kumpa nafasi ya kuongoza tena miaka mitano. "Uchaguzi umekwisha tunatakiwa kujenga nchi pamoja bila chuki wala hiana," alisema.

Mgombea urais kwa tiketi ya NCC- Mageuzi, Maganja alipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi huo.

Maganja alisema hakuna taifa wala taasisi ya nje, ambayo itangilia kupanga mambo ya nchi . Alisema taifa litaendelea kuwa moja na kusimamia mambo yake lenyewe. “Wagombea tulikuwa 15, sote tusingekuwa marais, lazima apatikane mmoja,” alisema.

Mgombea wa SAU, Mugahywa alisema NEC imesimamia uchaguzi kwa haki, uhuru na utulivu na matokeo yalitangazwa kwa muda mfupi, jambo ambalo linaweza kuwa rekodi ya dunia.

Alisema Rais Magufuli amejibeba mwenyewe, hakuna aliyembeba kutokana uzalendo wake kwa Watanzania, uadilifu na kazi alizofanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mugahywa alisema Magufuli amepata ushindi kutokana na kazi alizofanya ambazo zinajionesha wazi. “Na mahali pengine walikuwa wakisema sura ya hayati Mwalimu Nyerere imerudi kupitia Magufuli” alisema.

Mahona wa NRA aliipongeza tume kwa kuwa na ubunifu mkubwa na kuandaa uchaguzi vizuri kuanzia mchakato wa kuchukua fomu na hadi upigaji kura. Alimpongeza Magufuli kwa kuibuka kidedea na aliahidi kushirikiana naye.

Mgombea wa UMD, Mazurui wa UMD alisema anguko la wapinzani ni la haki, kwani uchaguzi ulikuwa wa huru na haki na Watanzania ni mashahidi.

Kwa mujibu wa Mazurui, anguko lao wameponzwa na baadhi ya wabunge wa upinzani, ambao hawakutekeleza ahadi zao kwa wananchi.

Alisema demokrasia si lazima chama kilichopo madarakani kishindwe, inaweza kuwa pia kutokana na wananchi kuridhika na sera zake ni chama kilichopo madarakani kuendelea kuongoza.

Mgombea wa ADC, Sendiga alimpongeza Rais Magufuli kwa ushindi na kwamba Watanzania wana imani naye kwamba ataendeleza maendeleo ya kiuchumi.

Aliwaonya wananchi wasiwasikilize wanasiasa, wanaowashawishi waingie mitaani na kuleta vurugu, Watanzania wanatakiwa kubaki wamoja na wala wasiyasikilize mataifa ya nje bali washikamane katika kuijenga nchi yao.

Alimuomba Rais Magufuli kutumia sera na baadhi ya hoja nzuri za wapinzani na kuziingiza katika ilani na kuzitumia kwa ajili ya kuleta maendeleo ya watanzania nchini.

Join our Newsletter