Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 05Article 513919

Siasa of Thursday, 5 November 2020

Chanzo: HabariLeo

Wamemkubali Magufuli tena, kazi inaendelea

Wamemkubali Magufuli tena, kazi inaendelea

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetuzwa ushindi wa kishindo na kukubaliana serikali yake iendelee kuisuka nchi kama inavyooneshwa katika Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025, hatua inayodhihirisha wananchi walivyoridhishwa pia na utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2015-2020.

Ushindi aliopata mgombea urais wa CCM, John Magufuli wa kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 mwaka huu pamoja na wa wabunge, unatajwa na watu wa kada tofauti kwamba ni uthibitisho kuwa wananchi wameelewa ilani na utekelezaji wa mambo mbalimbali aliyofanya katika miaka mitano ya uongozi wake wa kipindi chake cha kwanza.

Katika uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, Magufuli alipata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 na alitangazwa kuwa mshindi Oktoba 29 kabla kuapishwa Novemba 5 na kuanza rasmi kazi ya kuwatumikia wananchi katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano.

Miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 -2020 chini ya uongozi wa Rais Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, mafanikio makubwa yamepatikana katika nyanja na sekta zote za maendeleo kwa ustawi wa wananchi.

“Wananchi waliisoma Ilani ya CCM na kuielewa na kwa kuwa imeeleza mambo mengi yanayogusa maendeleo yao ndiyo sababu wameona wakipe nafasi chama hicho tena,” anasema Mbunge Mteule wa Jimbo la Mbarali, Francis Mtega.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu ushindi mkubwa wa CCM, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini alisema Watanzania wamependa maendeleo yaliyofanywa na Rais Magufuli.

Msomi na mwanadiplomasia, Dk Watengere Kitojo anamtaja Rais Magufuli kuwa chachu kubwa ya ushindi kutokana na alivyojitoa kwa dhati kuifanyia mambo makubwa katika kipindi cha miaka mitano.

Aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya ADC katika uchaguzi wa mwaka huu, Queen Sendiga anampongeza Rais Magufuli kwa ushindi akisema Watanzania wana imani naye kwamba ataendeleza maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema wanachama wafahamu kuwa huo ni mwanzo wa kazi, kutekeleza waliyowaahidi wananchi. “Ushindi huo ni dhamana ya kwenda kuchapa kazi,” alisema.

Pia Magufuli amethibitishia wananchi atakavyoendelea kuchapa kazi kwa nguvu akisema, ana deni kubwa kwao na atalilipa kwa kufanya kazi kwa bidii zaidi.

Alipokabidhiwa cheti cha ushindi wa uchaguzi wa rais mwanzoni mwa wiki hii jijini Dodoma, Rais Magufuli ambaye leo anaapishwa, alisema deni hilo ni kwa Watanzania kwa jumla waliompigia kura na ambao hawakumpigia.

Mafanikio 2015-2020

Miongoni mwa mafanikio yanayooneshwa katika ilani ni pamoja na serikali kuendelea kulinda na kuimarisha umoja, mshikamano, amani, utulivu, ulinzi na usalama, kuimarisha utumishi wa umma unaozingatia weledi, nidhamu, uadilifu, bidii na maarifa katika kazi.

Mengine ni kuimarisha mifumo ya kisera, kitaasisi na kisheria, ikiwemo kutungwa kwa sheria inayotaka serikali za mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake (asilimia 4), vijana (asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2).

Kuimarishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kulikowezesha kusimamia na kuboresha utendaji wa mashirika ya umma yaliyoweza kuchangia Sh trilioni 1.052 kama gawio na michango kwa serikali.

Kuhamishia Serikali Makao Makuu ya nchi Dodoma; kudhibiti na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu uchumi na ufisadi, na hivyo kuokoa fedha na rasilimali nyingine na kuzielekeza kwenye mipango ya maendeleo ya nchi.

Mengine ni kudhibiti na kuimarisha mapambano dhidi ya uzalishaji, uagizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya, utakatishaji wa fedha haramu na biashara ya kusafirisha binadamu.

Kujitosheleza kwa chakula na kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje; kuimarisha uchumi wa viwanda ambapo idadi ya viwanda imeongezeka kutoka viwanda 52,633 mwaka 2015 hadi kufikia viwanda 61,110 mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la asilimia 16.1.

Mafanikio mengine ni kutekeleza miradi ya kimkakati yenye tija kubwa katika uchumi na ustawi wa jamii ikiwamo, Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Mingine ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR); kufufuliwa kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya 11; kununua meli mbili mpya Zanzibar; na ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Serikali imeimarishwa mfumo wa udhibiti, usimamizi na umiliki wa madini na hivyo kuongeza mapato yatokanayo na mazao ya madini kutoka Sh bilioni 168 mwaka 2015 hadi Sh bilioni 517.57 mwaka 2020.

Mambo mengine ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya serikali kutoka wastani wa Sh bilioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa Sh trilioni 1.3 mwaka 2019.

Kwa upande wa Zanzibar, mapato ya serikali yameongezeka kutoka wastani wa Sh bilioni 428.5 mwaka 2015/2016 hadi kufikia Sh bilioni 748.9 mwaka 2018/19.

Matokeo ya mafanikio haya kwa maendeleo na ustawi wa wananchi kwa upande wa Tanzania Bara ni pamoja na wastani wa pato la mwananchi limekua kutoka Sh 1,968,965 mwaka 2015 hadi Sh 2,458,496 mwaka 2018, na Pato la Taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka.

Wastani wa umri wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 61 mwaka 2015 hadi miaka 65 mwaka 2020. Kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme kutoka megawati 1,308 mwaka 2015 hadi megawati 1,602.32 mwaka 2020. Vilevile, usambazaji wa umeme vijijini umeongezeka kutoka asilimia 16.4 mwaka 2015 hadi asilimia 67.1 mwaka 2020.

Serikali imetoa elimu bila malipo katika ngazi ya shule za msingi na sekondari na hivyo kuongeza udahili wa wanafunzi katika ngazi zote za elimu.

Idadi ya kaya zinazopata maji safi nchini kutoka vyanzo salama imeongezeka hadi kufikia asilimia 77 mwaka 2020. Vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka 7,014 mwaka 2015 hadi 8,446 mwaka 2020.

Kazi inaendelea

Ilani ya 2020-25 iliyonadiwa wakati wa kampeni na itakayotekelezwa chini ya Rais Magufuli, inasema katika miaka mitano ijayo, lengo la CCM ni kuendelea kustawisha maisha ya kila Mtanzania, kutokomeza umaskini na kuhakikisha kuwa taifa linafikia uchumi wa kati.

Katika kufikia lengo hili, vipaumbele vikuu vya serikali za CCM katika miaka mitano ijayo vitakuwa ni kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa.

Kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.

Serikali italeta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.

Itaimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini; kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi. Serikali itatengeneza ajira zisizopungua milioni saba katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.

Join our Newsletter