Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 20Article 515392

xxxxxxxxxxx of Friday, 20 November 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Wanasiasa mbaroni njama kulipua NEC, ZEC

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema jeshi hilo limewakamata viongozi wa vyama vya siasa kwa tuhuma za kufanya njama za kuvuruga Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

IGP Sirro pia alisema jana kuwa, pamoja na viongozi hao, watu wengine 254 wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa na jeshi hilo baada ya kusababisha vurugu katika maeneo mbalimbali nchini wakati wa mchakato wa uchaguzi na kuongeza kuwa watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wake kukamilika.

Aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa, viongozi hao wakiwemo kutoka Zanzibar na Tanzania bara, wanahusishwa kupanga mikakati ya kutaka kulipua visima vya mafuta na majengo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

IGP Sirro alisema baadhi ya watuhumiwa walikamatwa wakiwa na mabomu 11 yaliyotengenezwa kienyeji waliyokutwa nayo Zanzibar.

Alisema, kubainika kwao kulitokana na taarifa za kiitelejensia ambazo Polisi walipata mapema kabla watuhumiwa hawajatekeleza dhamira yao.

"Watuhumiwa wote bado wapo rumande tukiendelea kuwahoji na mara baada ya upelelezi kukamilika tutawafikisha mahakamani kwa ajili ya kwenda kujibu tuhuma dhidi ya mashitaka yanayowakabili," alisema IGP Sirro.

Alisema pamoja na kukamatwa kwa watu hao, matukio ya vurugu zilizojitokeza kipindi hicho cha uchaguzi zilisababisha vifo vya watu wawili akiwemo mmoja aliyeaga dunia Oktoba 26 Mkoa wa Kaskazini Pemba.

IGP Sirro alisema, mwingine alifariki dunia Oktoba 28 katika Mkoa wa Unguja, pamoja na askari aliyeuawa baada ya kuporwa silaha.

Alisema mwili wa askari huyo ulikutwa na kubainika kuwa kifo chake kilitokana na kuchinjwa. Kwa mujibu wa IGP Sirro silaha aliyokuwanayo ikipatikana ikiwa na upungufu wa risasi tisa kwa kuwa awali zilikuwa 30.

"Taarifa zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa kuna idadi kubwa ya vifo vilivyojitokeza wakati wa uchaguzi siyo za kweli zaidi zimelenga kuzua taharuki na kuichafua nchi yetu.

“Nawakaribisha waje ofisini na kutoa taarifa za vifo hivyo na ikiwezekana watupeleke walipozikwa nasi tutaomba kibali cha mahakamani tufukie miili hiyo na kujiridhisha," alisema IGP Sirro.

Alisema bado wanaendelea kuchunguza matukio yote ya Zanzibar wakati wa uchaguzi na kuongeza kuwa tayari amemuagiza Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai (DCI) afanye uchunguzi wa kina wa matukio hayo ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Kamanda Sirro aliwapongeza Watanzania hususani viongozi wa dini kwa kuwa mstari wa mbele kuliwezesha taifa kuvuka salama mchakato wa Uchaguzi Mkuu.

Alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha linakomesha matukio ya kihalifu yakiwemo ya kuchoma nyumba moto yanayoendelea kufanywa na kikundi cha kihalifu mkoani Mtwara na kudai kuwa tayari wanawashikilia watuhumiwa kadhaa kutokana na matukio hayo.

Kamanda Sirro alisema, wana taarifa kwamba, kikundi hicho pamoja na kuundwa na Watanzania kutoka mikoa ya Mtwara na Kigoma, pia kuna raia kutoka Kenya, Burundi, Rwanda.

Alisema ukiacha matukio hayo, hali ya usalama nchini ni shwari isipokuwa kuna ongezeko la matukio ya ulawiti na ubakaji Zanzibar na Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Join our Newsletter