Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2021 01 14Article 521117

Siasa of Thursday, 14 January 2021

Chanzo: HabariLeo

Wapanda miti Hospitali ya Uhuru kuenzi Mapinduzi ya Z’bar

Wapanda miti Hospitali ya Uhuru kuenzi Mapinduzi ya Z’bar

SHEREHE za miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zimefanyika mjini hapa kwa kupanda miti kuzunguka Hospitali ya Uhuru ya Chamwino.

Uopandaji miti huo uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge pamoja na viongozi wengine akiwemo, Katibu Tawala wa Mkoa, Maduka Kessy, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga pamoja na Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kutoka Ndaki ya Elimu.

Akizungumza baada ya kupanda miti, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, DK Mahenge alisema wanaungana na Wazanzibari katika kusherehekea mapinduzi yao kwa kuboresha, kulinda na kuhifadhi mazingira.

Dk Mahenge alisema mkakati wa kupanda miti kwa kila halmashauri milioni 1.5 unatakiwa usiwe wa kufuata matukio na sherehe, bali kuwa endelevu wakati wote.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy alisema kampeni ya kupanda miti ikidumishwa wakati wote Dodoma itakuwa ya kijani.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Mahenge kwa kuanzisha uhamasishaji upandaji miti kuzunguka hospitali hiyo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM), Godfrey Mabelle alisema vijana hao wapo tayari kutekeleza mapinduzi katika nchi kwa kuhakikisha wanasaidia kuiweka Dodoma ya Kijani wanapojiandaa kuwa viongozi wa kesho.

Diwani wa Kata ya Buigiri ilipo Hospitali ya Chamwino, Kenneth Yindi alisema ameipokea kampeni ya kupanda miti, iliyobaki ataisambaza katika vijiji jirani kuhakikisha wanakijanisha maeneo yao.

Yindi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chamwino, alisema kitendo cha kupanda miti kuzunguka Hospitali ya Chamwino kutasaidia wagonjwa kupata vivuli na matunda wanapokuwa wakipata huduma hospitalini hapo.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Chamwino Wilayani Chamwino, Godfrey Sollonga aliyeshiriki katika kampeni ya kupanda miti hiyo alisema mazingira ni uhai na kwa kupanda miti hiyo kutasaidia kuleta vivuli na misitu ambayo itatumika kwa shughuli nyingi baadaye zikiwemo kuni, mbao na matunda pamoja na mahitaji mengine.

Katibu Tawala Wilaya ya Chamwino, Juliana Kilasale alisema mkakati wao ni kuhakikisha upandaji miti inakuwa agenda ya kudumu kila wakati na kila taasisi lazima ipande miti kwa lengo la kusaidia kulinda, kuboresha na kuhifadhi mazingira.

Mwanafunzi wa UDOM, Ernester Sambo alisema wamejitokeza kupanda miti kwa sababu ya uzalendo wa nchi yao katika kulinda mazingira ya Hospitali ya Chamwino.

Join our Newsletter