Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 06Article 517457

Siasa of Sunday, 6 December 2020

Chanzo: HabariLeo

Wizara mpya yaakisi Ilani ya CCM

Wizara mpya yaakisi Ilani ya CCM

KUUNDWA kwa wizara mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kumeelezwa kutachochea ukuaji wa uchumi nchini unaotegemea kasi ya digitali.

Wachambuzi wanasema ukisoma kwa makini Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020-2025 utabaini CCM inataka kupeleka Tanzania katika uchumi wa kati wa viwanda unaogemezwa na uchumi wa kidigitali.

Wizara hiyo mpya ambayo itaongozwa na Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile inatarajiwa kuongoza katika mapambano ya kiuchumi ambayo kwa sasa katika dunia hii yanategemea na matumizi bora ya Tehama.

Jana Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akisoma Baraza la Mawaziri aliitaja wizara hiyo kuwa wizara pekee mpya iliyoundwa na Rais Magufuli. Katika mahojiano na Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Zainab Chaula alisema uamuzi huo ni wenye tija kubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.

Dk Chaula alisema kazi zilizoorodheshwa katika Ilani ya CCM ya 2020-2025 zinahitaji wizara hasa ikitambuliwa kwamba dunia sasa imekaa kidigitali zaidi. Kuanzishwa kwa wizara hiyo mpya kunakidhi matakwa ya Ilani ya CCM Sura ya Nne ambayo imeeleza kinagaubaga mahitaji makubwa ya kuwezesha Tanzania kuwa na Uchumi wa Kidijitali.

Katika kifungu cha 103 Chama Cha mapinduzi kimeelezwa kutambua uchumi wa kidigitali kuwa muhimu katika kuleta maendeleo kwa kuongeza ufanisi katika uzalishaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali na kutoa fursa za kuongeza vipato vya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa kuwa na wizara hiyo katika ulimwengu unaokwenda kasi na kutegemea zaidi teknolojia ya habari na mawasiliano, uundwaji wa wizara utahakikisha teknolojia mpya za kidijitali zinatumika kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Tanzania ikiwa inaelekea katika kuimarisha uchumi wake wa kati kutoka chini kwenda juu, ilani hiyo imeilekeza serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba kuna urahisishaji wa utoaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa umma kwa kuanzisha Vituo vya Huduma Pamoja ili kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali.

Wachambuzi wanasema kwa kuanzishwa kwa wizara hiyo ina maana kwamba taifa linataka kuongeza kasi katika kuhakikisha sayansi, teknoloja na ubunifu vinatumika kikamilifu katika kuendesha sekta za kukuza uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa hadhi ya kipato cha kati ambao ni shindani, jumuishi na unaoongozwa na viwanda.

Katibu Mkuu huyo akifafanua zaidi, alisema katika sekta ya mawasiliano kuna fursa nyingi ambazo zinapaswa kuendelezwa na kwa kuifanya kuwa wizara kamili inatoa mwanya wa utendaji kazi kuwa mzuri zaidi katika kuzitumia fursa hizo.

Alitolea mfano wa Mkongo wa Mawasiliano ambao umewekezwa na Serikali ya Tanzania kuwa ni kati ya vyanzo vikubwa vya mapato ambavyo vikiwa chini ya wizara kamili vitafanya kazi kubwa zaidi katika kuchangia pato la taifa.

Alisema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ujumla ina fursa nyingi na wizara itakuwa na jukumu kubwa la kuitendea haki sekta hiyo kwa faida ya taifa kwa ujumla. Dk Chaula alisema, “Ashukuriwe Rais wa uamuzi wake huu hakika ameona mbali katika kuhakikisha kuwa sekta hii ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inasonga mbele kwa kuiundia wizara yake.”

Ifahamike kuwa kwa sasa dunia nzima inawekeza kwenye sekta ya hiyo ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kwa serikali kuunda wizara kamili ya kushughulikia masuala haya inaonesha umakini wa hali ya juu katika kuzitumia fursa zenye kulenga kuliongezea taifa uwezo wa kukua kimipangilio katika dunia inayokwenda kasi kiteknolojia.

Join our Newsletter