Uko hapa: NyumbaniHabariMikoani2022 01 13Article 585586

Habari za Mikoani of Thursday, 13 January 2022

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Aliyeuawa kwa kukatwakatwa na mumewe azikwa

Aliyeuawa kwa kukatwakatwa na mumewe azikwa Aliyeuawa kwa kukatwakatwa na mumewe azikwa

Mamia ya wakazi wa Dodoma wamejitokeza kuuaga mwili wa Muuguzi wa Hospitali ya Taifa Mirembe, Rufi na Komba (37) aliyekufa baada ya kukatwa mapanga na mumewe na kisha kuchomwa moto.

Mwili wake umezikwa jana katika makaburi ya familia eneo la Miyuji Dodoma. Rufina alizaliwa Septemba 24, 1984 na kufa Januari 10, mwaka huu. Akizungumza kwenye msiba huo, Mwakilishi wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Matilda Limited alisema kada ya uuguzi imempoteza muuguzi mahiri mwenye ari ya kufanya kazi na mwenye ushirikiano mkubwa katika utendaji wa kazi.

Waombolezaji katika maziko hayo wameomba Jeshi la Polisi kumsaka na kumtia mbaroni mume wa Rufina ambaye ametoroka. Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa Afya wa hospitali hiyo, Dk Jackson Minja alisema tayari suala hilo liko mikononi mwa polisi ambao wanaendelea na uchunguzi juu ya mauaji hayo ya kikatili.

Dk Minja alisema wamesikitishwa na kitendo hicho cha mauaji ambapo hadi sasa hawajui chanzo ni nini isipokuwa wanasubiri ripoti ya uchunguzi kutoka Jeshi la Polisi ambalo linaendelea kufuatilia tukio hilo. Alisema walifika eneo la tukio kumtambua muuguzi huyo na kushuhudia akiwa na majeraha yaliyotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

“Tumeumizwa sana na kifo cha mfanyakazi mwenzetu, hatuna cha kufanya zaidi ya kusubiri taarifa ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa,” alisema Dk Minja wa Hospitali ya Mirembe. Alisema Rufina alisajiliwa Novemba 5, 2009 na ameacha watoto wawili wa kike. Alikuwa Katibu mwenezi kwenye Tawi la TANNA Mirembe. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga alisema atatoa taarifa kuhusiana na tukio hilo wakati wowote.