Uko hapa: NyumbaniHabariMikoani2021 08 17Article 551929

Habari za Mikoani of Tuesday, 17 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Bodi yashtuka uzalishaji mdogo wa Pamba

Uzalishaji Pamba Uzalishaji Pamba

WILAYA ya Maswa mkoani Simiyu inakabiliwa na tatizo la kushuka kwa uzalishaji wa zao la pamba kutoka kilo milioni 50, mwaka 2014 na kufikia kilo milioni 16 kwa mwaka 2021.

Kutokana na kuwapo tatizo hilo, Bodi ya Pamba imeamua kubuni kampeni ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Hayo yalibainishwa jana na Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk, wakati akiwasilisha mada kwenye kikao cha majumuisho ya mafunzo kwa viongozi wa ngazi ya wilaya, kata, vijiji na vitongoji yenye lengo la kuhamasisha uzalishaji wa zao hilo.

Alisema uzalishaji wa zao hilo unashuka mwaka hadi mwaka na kufanya wakulima wengi kukata tamaa ya kuendelea kulima zao hilo kwani wamekuwa wakipata hasara ukilinganisha na gharama za uzalishaji.

"Wilaya ya Maswa imekuwa ikishuka uzalishaji kila mwaka, wakulima wamekuwa wakitumia gharama kubwa katika uzalishaji, lakini hawazalishi kwa tija...wilaya haiendi mbele badala yake inashuka kwa uzalishaji kwa kasi na kwa kuliona hilo tumeamua kuja na mkakati kabambe wa kuongeza tija," alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge, alisema  hayupo tayari na hataruhusu kuona wilaya yake inashuka tena kwenye uzalishaji wa pamba.

Alisema atahakikisha anasimamia vyema lengo lao la kuzalisha tani 130,000 huku akiwatahadharisha watendaji wa kata, vijiji na maofisha ugani watakaozembea kutekeleza maagizo na makubaliano waliyojiwekea.