Uko hapa: NyumbaniHabariMikoani2021 11 25Article 574048

Habari za Mikoani of Thursday, 25 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Bomoabomoa Mbweni yapigwa 'stop'

Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa DSM. Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa DSM.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesitisha bomoabomoa iliyokuwa inaendelea maeneo ya mpakani mwa Bunju na Mbweni.

Amechukua uamuzi huo jana Novemba 24,2021 alipotembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi.

Siku mbili zilizopita wakazi wa eneo hilo walieleza kupambana na polisi na maofisa ardhi waliofika kubomoa nyumba zao na kueleza kuwa hayakuwa maagizo ya mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe waliyokubaliana naye katika kikao chao cha kulijadili suala hilo.

Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza malalamiko, Makalla amesema ubomoaji huo usitishwe kwanza na hakuna atakayeruhusiwa kujenga chochote kwa sasa hadi hapo timu yake itakapofika na kusikiliza mapendekezo ya wananchi yatakayowasaidia kutoa uamuzi kwa maslahi ya pande zote.

Pia, alinuaguza mkuu wa kituo cha polisi Mbweni kuhakikisha polisi wote walioshikiliwa katika kituo cha polisi kutokana na kuibuka kwa mgogoro huo kuachiwa.

Mmoja wa wakazi hao, Mwajuma Mfaume amesema kwa kuwa baadhi walishaendeleza kwa kujenga nyumba za kudumu, wanaiomba Serikali iwafikirie kuwapa maeneo kabla ya kuwahamisha, lakini wakashangaa ubomoaji wa kutumia mabavu ukifanyika.

Mkazi mwingine, Eva Mathias amesema hivi sasa upimaji unaofanywa wa viwanja katika eneo hilo ni mita za mraba 50 kwa 50 na malipo yake ni fedha nyingi ambazo wao hawawezi kumudu lakini kwa kuwa walishajenga, alishauri Serikali iangaliwe namna wapimiwe vipimo watakavyovimudu wananchi wa hali ya chini.

Salum Hashim, amesema walipewa eneo hilo mwaka 2005 kwa ajili ya shughuli za kilimo na wafugaji lakini baadaye Serikali ikalitwaa na kukata viwanja na hata mgogoro wa juzi ulivyoibuka waliahidiwa kuwa waandike namba kwa ajili ya kutafutiwa maeneo mengine.

“Lakini ndio tunashangaa kilichofanyika ni kuja kubomolewa nyumba na kupigwa mabomu yaliyosababisha wengine kulala nje na watoto hadi leo na wengine wakiwa wanashikiliwa na jeshi la Polisi,” amesema Hashim.

Awali Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Idrisa Kayera amesema eneo hilo Serikali ilichukua kwa wananchi na kuwalipa fidia licha ya kuwa zilichelewa kutolewa jambo lililochangua watu wengine kuvamia baadaye.

Amesema hivi sasa wameamua kuliendeleza eneo hilo kwa kurudisha alama ambazo wananchi walizing'oa ili kuanza kuuza viwanja hivyo ambapo fedha zake walizikopa na wanatakiwa kuzirejesha.

Akizungumza namna walivyopokea maamuzi ya Makalla, fredrick Edward ambaye ni kiongozi wa wananchi hao amesema ni jambo zuri kwani kuna wananchi 186 mpaka sasa wameathirika na bomoabomoa hiyo huku nyumba 59 zikiwa zimebomolea.