Uko hapa: NyumbaniHabariMikoani2021 08 18Article 552067

Habari za Mikoani of Wednesday, 18 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Dkt. Mahenge aagiza kila idara kukusanya mapato yake

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mkuu wa Mkoa wa Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk Binilith Mahenge ameagiza kila mkuu wa Idara kwenye halmashauri za mkoa huo kuhakikisha anashiriki katika kupanga na kukusanya mapato ya idara yake badala ya kuachia jukumu hilo kwa wakurugenzi na wakusanya ushuru.

Alisema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha isiyo ya lazima, hivyo kuinua kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.

Dk Mahenge alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Ikungi ambapo alibaini kuwa wengi wa wakuu wa idara katika halmashauri hiyo hawakuwa wanajua chochote kuhusu kiwango cha ushuru kilichokusanywa kwenye maeneo yao.

"Kuanzia sasa kila mkuu wa idara ajue ya mapato ya eneo lake. Inaelekea suala la ukusanyaji mapato kaachiwa Mkurugenzi Mtendaji na wakusanya ushuru tu kwani kila mkuu wa idara ninayemuuliza hapa, eti hajui!" aliagiza.

Alisisitiza kuwa suala la ukusanyaji mapato halina budi kutiliwa mkazo wa aina yake na kusimamiwa kikamilifu kutokana na ukweli kwamba mapato yanapoongezeka yanaleta heshima kwa halmashauri husika na mkoa kwa ujumla, lakini pia hupunguza utegemezi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Justice Kijazi alisema hadi Julai 31 mwaka huu, halmashauri hiyo ilipokea na kukusanya Sh bilioni 2.14 kutokana na bajeti ya Sh bilioni 38.79 ambayo ni sawa na asilimia sita.

Alifafanua kati ya kiasi cha fedha kilichopokelewa, Sh milioni 142,70 ni mapato ya ndani, Sh bilioni 1.69 ni mishahara, Sh milioni 207.38 ni fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh milioni 104.86 ni fedha za elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari.

Hata hivyo, alisema kuwa mapato ya ndani halisi kwa kipindi hicho yalikuwa Sh milioni 117.0 ambayo ni sawa na asilimia saba ya bajeti.