Uko hapa: NyumbaniHabariMikoani2021 09 15Article 557500

Habari za Mikoani of Wednesday, 15 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Hizi ndio kero 500 zilizofika mikononi mwa RC Makalla 

Hizi ndio kero 500 zilizofika mikononi mwa RC Makalla  Hizi ndio kero 500 zilizofika mikononi mwa RC Makalla 

WIKI moja iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla, amekuwa na ziara katika majimbo matano ya mkoa wake yakiwemo ya Kawe, Kibamba, Segerea, Mbagala na Kigamboni.

Lengo la ziara hiyo ni kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi katika maeneo hayo na kuzipatia ufumbuzi ambapo kati ya kero zaidi ya 500 alizozisikiliza nyingi zilihusu migogoro ya ardhi pamoja na mirathi.

Katika ziara hiyo wananchi wengi waliweza kujitokeza kwa ajili ya kutoa malalamiko yao kwa Mkuu huyo wa Mkoa ili ziweze kupatiwa suluhisho la kudumu.

Pamoja na kusikiliza kero za wananchi Makalla amekuwa akitoa angalizo kwa kero ambazo tayari zimefikishwa mahakamani kuwa hawezi kuziingilia anaiachia mahakama ifanye uamuzi ila anachoweza kusaidia ni kutoa msaada wa kisheria kupitia watendaji wake.

Sehemu ya kwanza ya ziara hiyo ya Makalla ilikuwa ni Jimbo la Kawe ambapo pale pamoja na kero mbalimbali zilizowakabili wananchi aliwaambia kuwa serikali ilitoa sh bilioni 24 zitakazotumika kukabiliana na changamoto za miundombinu ya barabara jimboni humo.

Kwa maelezo ya Mkuu huyo wa Mkoa, fedha hizo zimetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa bwawa la mvua, ujenzi wa barabara ya viwango vya lami na changarawe kwenye maeneo mbalimbali.

Hivyo aliwaagiza watendaji wa wilaya ya Kinondoni kusimamia fedha hizo kwa kuwa tayari zipo kwenye manunuzi ya vifaa mbalimbali vya ujenzi.

Akifafanua hilo anasema “Nimefika mahali hapa na ofisi inayotembea kwa maana nipo na maofisa wangu mbalimbali watakaosaidia kutatua kero za wananchi,”.

Katika Jimbo hilo la Kawe, Mbunge Josephat Gwajima alieleza kero za eneo hilo kuwa ni barabara kwa kuwa nyingi ni mbovu pamoja na mafuriko katika eneo la Bunju, Wazo na Kawe.

Katika siku ya pili Makalla alitembelea Jimbo la Kibamba ambapo Mbunge wa Jimbo hio Issa Mtemvu aliomba wajasiriamali wajengewe vibanda vya biashara kando kando ya barabara ya njia nane ya kutoka Kimara hadi Kibaha.

Kuhusu hilo, Makalla anaeleza kuwa ajali nyingi na foleni zilizopo katika mkoa wake zinachangiwa na ufanyaji wa biashara holela katika maeneo ya wazi.

“Tuna biashara holela kila mahali, leo foleni tunapata kwa ajili ya biashara holela. Biashara holela imekuwa kero sasa hivi kupita sehemu yoyote ni sahihi.

“Barabara zetu kumekuwa na foleni kwa sababu kila kwenye upenyo ama kwenye kuchepuka mtu anapanga vitunguu,” anasema.

Akiwa katika Jimbo la Segerea Makalla aliagiza Mamlaka ya Maii Taka na Safi (Dawasa), kupiga kambi katika eneo la Buguruni ambalo wananchi wake wanalalamikia kukerwa na mfumo wa maji taka uliopo.

“Naelekeza Dawasa tupige kambi Buguruni muangalie mfumo wa maji taka na kuufanyia maboresho,” anasema.

Agizo hilo amelitoa baada ya mkazi wa eneo hilo, Salum Chande kutoa malalamiko ya kufurika kwa maji taka katika eneo hilo kwa kipindi cha miaka 10 bila kupatikana kwa suluhisho la kudumu.

Maelezo ya mkazi huyo ni kwamba, mifumo ya maji taka imekuwa ikitiririka mitaani kutokana na Dawasa kushindwa kutatua changamoto hiyo.

Hivyo baada ya kupewa agizo hilo na Mkuu wa Mkoa, Ofisa kutoka Dawasa Burton Mwalupaso aliahidi kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi.

Pia Makalla akiwa katika Jimbo hilo la Segerea amepiga marufuku michango inayoendelea kwenye shule za serikali mpaka hapo atakapotoa kibali chake.

Lakini amekataza biashara zinazofanywa pembezoni mwa shule ili kuwawekea mazingira mazuri watoto ya kusoma.

Katozo hilo alilitoa baada ya mwananchi mmoja Abinani Lukwale kueleza kuwa michango imezidi kuwa mingi shuleni na mingine wasipotoa watoto hurudishwa nyumbani au kunyimwa kufanya mitihani ambapo kila siku hutakiwa kutoa sh 300 na Jumamosi sh 1000.

Akifafanua hilo anasema, “Kuanzia sasa napiga marufuku michango hiyo mpaka pale itakapopata ridhaa yangu.

“Kwa michango hii kama shule ina wanafunzi 2000 ina maana shule inakusanya sh 600,000 na hapo bado sh 1000 ambazo wanazikusanya kila Jumamosi.

“Ukweli ni kwamba michango hiyo huwaongezea mzigo wazazi wakati serikali imeshaamua kutoa elimu bila malipo, hii sitakubali ndani ya uongozi wangu,” anasema.

Kutokana na hilo anasema kuanzia sasa michango yoyote lazima iidhinishwe nay eye mwenyewe na hiyo ni baada ya kikao cha wazazi na uongozi wa shule kuridhia kama ambavyo muongozo wa elimu unavyoelekeza.

Kuhusu biashara hizo zinazofanywa pembezoni mwa shule amezikataza badala yake anataka kuwekwe utaratibu wa watu watakaotambuliwa na uongozi wa shule kufanya biashara zao ndani ya shule hizo.

Hivyo ameagiza watendaji kusimamia hilo kwa kutoa elimu na kuweka vibao vya makatazo kwa kusema kuwa hali imekuwa mbaya kwa sasa katika shule nyingi kutokana na kufanyika kwa biashara holela.

Katika Jimbo la Mbagala, Makalla anaagiza wafanyabiashara kuondoka katika eneo la mradi wa ujenzi wa mwendokasi uliopo eneo hilo ili kuruhusu ujenzi huo kuendelea bila vikwazo ikiwa ni pamoja na kuepusha ajali inayoweza kutokea.

Mradi huo wa mwendokasi wenye kilomita 12.3 unagharimu sh bilioni 217.

Agizo hilo analitoa kwa mara nyingine ili wafanyabiashara hao sasa waondoke kabla ya hatua nyingine za kisheria hazijachukuliwa.

Makalla anasema kitendo cha wafanyabiashara hao kubaki kunasababisha wakandarasi kulalamikia jambo hilo ambalo ni hatari kwa afya za wafanyabiashara hao kwani ujenzi unapoendelea unaweza kusababisha majeraha na vifo.

Katika Jimbo la Kigamboni serikali inaendelea kusimamia mradi mkubwa wa maji ya kisima wa Kimbiji wenye thamani y ash bilioni 24.7 katika eneo la Kigamboni ili kuwawezesha wananchi kutokupata changamoto hiyo.

Makalla anasema lengo la serikali ni kuhakikisha maji hayo yanafika katika kata zote za jimbo hilo na kwamba mpaka sasa umefikia asilimia 30, mradi huo unajengewa matenki ya lita milioni 15, pampu 10 za kufungwa maji yanayokwenda kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa maji kwenye visima.

Makalla anasema mradi huo utakamilika ifikapo April Mwaka ujao.

Lakini pia alitoa onyo kwa watu wanaojulikana kama vishoka wa ardhi kuacha utapeli kwa wananchi na kuwasababishia hasara.

Kwa maelezo ya Makalla vishoka hao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ili kudhulumu mali za watu ikiwemo mihuri feki, picha za viwanja visivyo vyao na kutumia nakala za uongo katika biashara hiyo.

Hivyo ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa ni faraja kwa wakazi wa Dar es Salaam kwa kuwa wengi wao wameweza kutatuliwa kero zilizokuwa zikiwasumbua ama kupata mwongozo wa nini kifanyike changamoto zao ziishe.

Hakuna shaka kuwa hicho alichokifanya Makalla kitafanywa na watendaji wake wengine mbalimbali ili atakaporudi tena kwa wananchi katika Jimbo lake yasiwepo malalamiko.