Uko hapa: NyumbaniHabariMikoani2021 09 14Article 557302

Habari za Mikoani of Tuesday, 14 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

RC Mtaka awapa mbinu viongozi wa dini kujiongezea kipato

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amewashauri viongozi wa dini kutumia fursa zilizopo mkoani humo kuanzisha miradi itakayowaongezea kipato badala ya kutegemea sadaka na michango ya waumini.

Alitoa ushauri huo juzi wakati akizungumza na viongozi pamoja na waumini wa dini mbalimbali kwenye uzinduzi wa hoteli ya kisasa ya Maniyanguru iliyopo Makulu, Dodoma. “Nawashauri viongozi wa dini kutumia fursa ya kuanzisha miradi itakayowaweza kuwainua kiuchumi badala ya kutegemea michango na sadaka.

Wekezeni miradi mbalimbali kama vile; kilimo,ufugaji ujenzi wa vitega uchumi kama vile hoteli za kisasa na majengo ya kulala wageni,” alisema. Aliwataka viongozi hao kuwa mfano kwa waumini wao wanaowasimamia kwa kufanya kazi za mikono, badala ya kuishia kuwahubiria huku wakiendelea kuwa masikini kwenye maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Mmiliki wa hoteli hiyo ya Maniyanguru, Askofu Livingstone Denis, alisema hadi kukamilika kwa ujenzi wake, zaidi ya Sh milioni 500 zimetumika. Alisema mafanikio hayo yametokana na kuwekeza kwenye kilimo na ufugaji ambao umemfanya kujiinua kiuchumi na kumwezesha kujenga hoteli hiyo ya kisasa pamoja na kuwa yeye ni kiongozi wa dini.

Askofu huyo wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAG), wilayani Kongwa katika Mkoa wa Dodoma, pia aliwashauri viongozi wa madhehebu ya dini kufanya kazi za mikono zenye tija zitakazowaletea maendeleo badala ya kutegemea ufadhili ikiwemo michango na sadaka kutoka kwa waumini. Alisema pamoja na kazi ya kiutumishi waliyonayo pia wanatakiwa kujishughulisha katika kufanya kazi kwa mikono yao na kuibua miradi ambayo itawainua kiuchumi.