Uko hapa: NyumbaniHabariDini2021 06 10Article 541975

xxxxxxxxxxx of Thursday, 10 June 2021

Chanzo: ippmedia.com

Wajasiriamali waomba kuwezeshwa mitaji

Mwenyekiti wa kikundi cha wajasiriamali cha Tusumuke jijini Dodoma, Chritopher Dioniz, alisema hayo jana jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema suala la mitaji kwa wajasiriamali nchini bado ni kikwazo kikubwa kufikia katika malengo yao ya kibiashara.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa hivi sasa wana soko kubwa la bidhaa wanazozitengeneza, lakini kikwazo ni idadi ndogo ambayo haikidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.

“Tunaiomba serikali yetu tukufu itushike mkono ili tupate mitaji ambayo itatuwezesha kuzalisha kwa kiwango kikubwa bidhaa zetu ili kukidhi mahitaji ya soko lililopo hivi sasa,” alisema Dioniz.

Alisema serikali inatakiwa kuvitumia vikundi vya wajasiriamali na kuviwezesha kutengeneza umoja ambao utasaidia kuwa na bidhaa za kutosha katika soko.

“Sisi hapa tunauza vifaranga vya kuku wakati mwingine unapata oda ya mteja, lakini unakua huna vifaranga wa kutosha kama vikundi vitatengeneza mnyororo wa kushirikina kwa pamoja kila kikundi kitakuwa na jukumu la kuzalisha bidhaa kwa mujibu wa mahitaji ya soko,” alisema.

Naye, Mariam Said, msindikaji wa bidhaa za vyakula jijini Dodoma, alisema kuwa wanakabiliwa na tatizo la vifungashio pamoja na kulifikia soko la nje.

Alisema hivi sasa wasindikaji wa bidhaa za vyakula nchini wanatumia vifungashio kutoka nje ya nchi kutokana kukosekana vyenye ubora nchini.

“Hivi sasa vifungashio tunachukua nchini Kenya ambavyo ndivyo vyenye ubora ukilinganisha na vya hapa kwetu,” alisema.

Alisema kutokana na tatizo la ugonjwa wa corona kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa vifungashio kutokana na mipaka mingi kufungwa.

“Tunaiomba serikali yetu kulifanyia kazi suala hili ili kupata wawekezaji wengi watakao wekeza katika viwanda vya utengenezaji wa vifungashio vyenye ubora vitakavyo wezesha bidhaa zetu kuingia katika ushindani wa soko la dunia,” alisema.

Join our Newsletter