Uko hapa: NyumbaniDini2021 08 12Article 551071

Dini of Thursday, 12 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Viongozi wa dini waelekeza mambo 10 kukabili corona

Viongozi wa dini waelekeza mambo 10 kukabili corona Viongozi wa dini waelekeza mambo 10 kukabili corona

VIONGOZI wa dini wametoa tamko lenye mambo 10 ya kutekelezwa na vyombo vya dini nchini katika kupambana na ugonjwa wa homa ya kali ya mapafu (covidi-19) unaosababishwa na virusi vya corona.

Baadhi ya mambo hayo ni kuipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kuwaletea wananchi chanjo dhidi ya ugonjwa huo na kupanga siku moja ya kufanya ibada ya kitaifa kumuomba Mungu aipushie nchi na janga hilo la covid -19.

Tamko hilo liliwasilishwa kwa niaba ya viongozi wengine wa dini, jijini Dar es Salaam jana na Katibu wa Baraza la Ulamaa na Msemaji wa Mufti wa Tanzania, Shehe Hassan Chizenga.

Alisema kutokana na janga la covid 19 viongozi wa dini kwa pamoja na vyombo vyao vya dini wanatakiwa kutekeleza mambo hayo 10, ikiwamo taasisi zote za dini kuweka vifaa vya kunawia mikono na kuwa na maji tiririka katika nyumba za ibada na waumini wote kuvaa barakoa wawapo katika maeneo ya ibada.

"Hapa tumekubaliana pia kuhakikisha waumini wetu wanakaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya muumini mmoja na mwingine na ikiwezekana kuweka alama kwenye viti au mikeka kuonesha mtu mmoja baada ya mwingine anapostahili kukaa umbali na mwenzake," alisema Shehe Chizenga.

Alisema pia wamekubaliana kufanya usafi katika nyumba za ibada kabla na baada ya sala, wazee na watoto na wenye matatizo ya kiafya walio hatarini kupata maambukizi ya corona kutohudhuria mikusanyiko ya ibada na kutoa mara kwa mara elimu kuhusu covid 19.

Alisema pia wamekubaliana nyumba za ibada zikiwa finyu uanzishwe utaratibu wa kusali maeneo ya wazi na kuongeza idadi ya ibada ili kupunguza msongamano, huduma zinazohusisha kugusana katika masuala ya dini ziepukwe na ibada zote ziwe na muda mfupi usiozidi saa mbili.

"Lakini pia tumekubaliana viongozi wa dini kuishukuru serikali kwa hili la kuwaletea Watanzania chanjo. Hili ni jambo jema lenye nia ya kuwakinga na halipingani kabisa na misingi ya dini zetu," alisema.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima alisema bado hali ya maambukizi nchini na duniani kote ya ugonjwa huo si nzuri na kwamba jitihada za udhibiti wa maambukizi yake zinahitaji kupewa kipaumbele.

"Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni nne hadi sasa duniani wamepoteza maisha kwa corona na kwa nchi za Afrika ni zaidi ya watu 100,000. Serikali yetu imechukua hatua za kuhakikisha wananchi wanaendelea kufuata ushauri wa kitaalamu ikiwamo kuendelea kutumia tiba za asili," alisema.

Dk Gwajima alisema awali serikali iliruhusu matumizi ya tiba za asili baada ya kuona duniani kote ugonjwa huo ulikuwa hauna tiba wala kinga. "Nasisitiza bado tiba asili ni zana sahihi za mapambano dhidi ya vita hii," alisema.

Kuhusu chanjo, Waziri huyo alisema mwamko wa Watanzania kwenda kuchanjwa ni mkubwa na serikali imeanzisha vituo 550 nchi nzima vinavyotoa huduma hiyo ya chanjo.

"Kwa sasa tuna dozi milioni moja na nusu ya chanjo ikiwa ni msaada kutoka Marekani. Nchi nyingi zimejitokeza kutaka kutusaidia nazo zitaleta chanjo ikiwamo China. Tunahamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kuchanja na waachane na taarifa potofu na badala yake watafute taarifa sahihi kutoka kwa watalaamu," alisisitiza na kuongeza:

"Suala la watu kudai kuwa chanjo hizi zimetengenezwa haraka halina msingi kwani hivi sasa kuna ukuaji wa teknolojia mambo yanakwenda kwa haraka."

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Profesa Abel Makubi aliwaomba viongozi wa dini kutumia ushawishi wao kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya corona pamoja na kwenda kuchanjwa.

"Nasisitiza tuepuke misongamano isiyo ya lazima ibaki ambayo itaendelea kwa sababu ya maisha ya wananchi. Twendeni tukachanjwe huku tukichukua tahadhari. Chanjo ni muhimu, serikali haiwezi kushawishi umma kutumia chanjo ambayo haina uhakika nayo," alisema Profesa Makubi.