Uko hapa: NyumbaniDini2021 11 24Article 573826

Dini of Wednesday, 24 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Wachungaji KKKT wamgeuka Askofu Shoo

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo

Siku chache baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dk Fredrick Shoo kuagiza kiti cha Askofu Dk Edward Mwaikali kurejeshwa Dayosisi ya Konde Tukuyu, wachungaji wa majimbo matano kati ya saba wamepinga maagizo hayo.

Novemba 16, Dk Shoo alifanya ziara mkoani hapa kufuatia mgogoro wa kanisa hilo baada ya waumini kumtuhumu Askofu Dk Mwaikali kuhamishia mali za kanisa na kuzipeleka makao makuu ya Konde jijini Mbeya.

Katika kikao kilichofanyika Tukuyu, kilichowahusisha viongozi wa Serikali, akiwamo Kamanda wa Polisi Mkoa, Urlich Matei na Msajili wa jumuiya za dini kilicholenga kumaliza mgogoro huo, Dk Shoo aliagiza hadi kufikia Novemba 22 kiti cha Askofu kirejeshwe Dayosisi ya Tukuyu, ambapo wachungaji wameweka ngumu wakidai hawakufurahishwa na vitendo vya kiongozi huyo.

Wakizungumza jana jijini Mbeya kwenye kikao kilichohusisha wachungaji 67 kutoka majimbo matano kati ya saba, walisema hawakubaliani na uamuzi ya Dk Shoo kwa kuwa amelifedhehesha kanisa na viongozi wao.

Nyibuko Mwambola, mchungaji wa jimbo la Mbeya Mashariki amesema hawakubaliani na ubabe, uonevu na unyanyasaji aliofanyiwa Askofu Mwaikali.

Amesema hawakutarajia vyombo vya dola vitumike kuwalazimisha viongozi wa Dayosisi kufika kituo cha Polisi ili kukutana nao kwa mazungumzo badala ya kutumika kwa ofisi ya Dayosisi.

Agosti 22, 2021 waumini wa kanisa la KKKT Dayosisi ya Konde Tukuyu walifanya vurugu wakipinga Askofu Mwaikali kuhamisha mali za kanisa hilo kuzipeleka makao makuu ya Ruanda Mbeya hadi Jeshi la Polisi lilipoingilia kati.