Uko hapa: NyumbaniMichezoMpira wa Miguu2021 11 23Article 573724

Soccer News of Tuesday, 23 November 2021

Chanzo: habarileo

Kagere ataka kiatu cha dhahabu

Kagere ataka kiatu cha dhahabu Kagere ataka kiatu cha dhahabu

MSHAMBULIAJI wa Simba, Meddie Kagere ambaye hivi sasa anaongoza katika orodha ya wafungaji kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara akiwa na mabao manne amesema kuwa lengo lake msimu huu ni kuweka rekodi ya ufungaji bora kwa mara ya tatu.

Kagere ameanza vyema kampeni ya kusaka kiatu cha ufungaji baada kufunga mabao manne hadi sasa na kuisaidia Simba kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 14, nyuma ya Yanga wanaoongoza.

Akizungumza na gazeti hili, Kagere alisema kuwa malengo yake ni kuisaidia Simba kutetea taji la Ligi Kuu kwa mara ya tano, lakini akili na nguvu ameihamishia katika kukisaka kiatu cha dhahabu ili aweke rekodi ya kuchukua kiatu hicho kwa mara ya tatu akicheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Wakati nakuja Tanzania ndoto yangu ilikuwa ni kuisaidia timu yangu kushinda makombe, lakini pia kiu yangu ilikuwa kuwa mfungaji katika Ligi jambo nililolifanya mara mbili na hivi sasa nataka kuchukua tena kwa mara ya tatu.”

"Msimu uliopita sikuwa napata nafasi ya kucheza mara kwa mara, msimu huu umeanza vizuri malengo yangu ni kuona kwamba ninaweza kuchukua kiatu cha ufungaji na inawezekana kama tutaendelea kupeana ushirikiano, huu ni mwanzo tu naamini kuna mengi mazuri yanakuja,” alisema Kagere.

Raia huyo wa Rwanda alijiunga na Simba msimu wa 2018/19 akitokea Gor Mahia ya Kenya na kuwa mfungaji bora msimu wake huo wa kwanza pamoja na wa pili 2019/20.

Kagere katika misimu minne aliyocheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, amefunga mabao 62 baada ya kucheza michezo 77.