Uko hapa: NyumbaniMichezoMpira wa Miguu2021 09 10Article 556543

Soccer News of Friday, 10 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Manara aambiwa aweke akiba ya maneno

Manara aambiwa aweke akiba ya maneno Manara aambiwa aweke akiba ya maneno

HIVI karibuni Haji Manara aliyekuwa Msemaji wa Simba aliajiriwa kwa watani zao Yanga, lakini wanachama wamemwambia aweke akiba ya maneno.

Hayo yametamkwa na uongozi wa tawi la Simba la Mpira Biriani, lililopo Buza Nyama Choma, gazeti hili lilipotembelea tawi hilo na kukutana na viongozi waliomtaka Manara apunguze maneno dhidi yao na kumtaka ubinadamu badala ya kejeli.

Msemaji wa tawi hilo, Mrengo Mkayala alisema Simba ni klabu kubwa, inaweza ikafanya mabadiliko ya aina yoyote ile na ikaendelea kusonga mbele, inapotokea mtu anaikashifu, huku akisema alipoenda wanamwona kama msaliti.

“Mfano mzuri hapo zamani ilionekana hakuna mchezaji kama Emmanuel Okwi, viongozi wakajipambanua wakajifunza kusajili wachezaji wenye tija na eneo hilo kwasasa linaendelea vizuri, hivyo Manara asiseme anaipenda Simba wakati tuliokuwa tunamuunga mkono wakati wa majukumu wake anatukashifu,” alisema.

Aliendelea kusema kama Manara amekwenda Yanga kwa sababu ya kazi, alimshauri afanye kazi yake na aachane na Simba.

Naye Katibu wa tawi hilo, Mohammed Mbonde alisema Simba inachotakiwa kukifanya kwasasa ni kuonyesha vitendo vyenye tija ya maendeleo ya soka, badala ya kujibizana na kelele kama zinazofanywa na Yanga.

“Tunajua Yanga inachekelea kinachofanywa na Manara, tunawaacha wajisahau na hilo, ila viongozi wetu wanapaswa kuweka nguvu zaidi kwenye maandalizi ya kikosi imara, hilo ndilo la msingi kwetu na ndilo litafanya tuje tufikie maendeleo kama ya TP Mazembe,” alisema.

Mwanachama wa tawi hilo, Nuru Khatibu aliunga mkono hoja hiyo ilipofikia klabu yao hadi Al Ahly imeweza kuona mchezaji anayeweza kuendana na thamani ama ubora wao, wanapaswa kufanya vitu vya maendeleo badala ya maneno mengi.

“Manara amekwenda kwenye timu inayopenda maneno badala ya kufanya maendeleo, viongozi wa Simba watazame mbele, ili wamwonyeshe kwa matendo na siyo kujibizana naye,” alisema.

SAFU UONGOZI

Tawi hilo lenye wanachama 59, linaongozwa na Mwenyekiti wa muda, Juma Omary ‘Kizingiti’, Katibu Mbonde, Mtunza Hazina Time Hilali anasaidiana na Mrengo Mkayala.