Uko hapa: NyumbaniMichezoMpira wa Miguu2021 10 10Article 562375

Soccer News of Sunday, 10 October 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Nabi apangua jeshi upyaaa.. awapa kina Mayele mechi mbili!

Kocha Nasreddine Nabi, akitoa maelekezo kwa wachezaji Kocha Nasreddine Nabi, akitoa maelekezo kwa wachezaji

Kocha Nasreddine Nabi aliamua kuizuia kambi ya Arusha kwa timu yake na fasta akaamua kulipanga upya jeshi lake kwa mechi mbili muhimu za Ligi Kuu Bara mikoani, akisisitaka anataka kubeba pointi sita, akiamini zitawafanya kina Fiston Mayele na wenzake kurudi na moto na kutupia mabao ya kutosha.

Yanga ilipanga kwenda kuweka kambi jijini Arusha katika akademi ya Black Rhino, iliyopo Karatu lakini Kocha Nabi akazuia akisema hataki wachezaji wake wasumbuliwe kwa sasa na badala yake kambi itakuwa Dar es Salaam na katika kuhakikisha wanakuwa fiti zaidi .

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo anayesaidiana na Cedric Kaze na Razak Siwa, alisema wameona waendelee na kambi yao wakijifua, lakini anataka mechi mbili za kirafiki kabla ya kuwafuata KMC mjini Songea mkoani Ruvuma kucheza nao Oktoba 19 kisha kusafiri hadi Arusha kumalizana na Azam FC.

Mechi yao na Azam itapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha siku ya Oktoba 30, Yanga ikiwa wenyeji na Kocha Nabi amesisitiza katika mechi hizo zote anataka kuvuna alama ili kujiweka pazuri kwenye ligi hiyo ambayo kwa misimu minne mfululizo bila kutwaa ubingwa.

“Tumeona bora tubaki Avic kwa maandalizi ya michezo yetu ijayo kwa kuivaa KMC kisha ratiba nyingine ziendelee,” alisema Nabi aliyeiwezesha Yanga kubeba Ngao ya Jamii kwa kuilaza Simba bao 1-0 Septemba 25.

Mechi ya Yanga na KMC imekuwa na vuta ni kuvute huku msimu uliopita mchezo wao wa kwanza walitoka sare 1-1. Kwenye mechi ya pili Yanga ilishinda 2-1.

BODI YAFAFANUA

Ishu ya timu za Ligi Kuu kuamua kubadilisha viwanja katika baadhi ya mechi zao za nyumbani, zimekuwa zikiwachanganya mashabiki wa soka na jana Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi (TPLB) ilitoa ufafanua na kuthibitisha kupokea ombi la klabu ya KMC kucheza mechi yao na Yanga kwenye Uwanja Majimaji mkoani Ruvuma badala ya uwanja wa Uhuru, Dar kama ilivyokuwa kwenye ratiba ya Ligi.

Yanga nao iliyokuwa iwe wenyeji wa Azam jijini Dar es Salaam wamesema mechi yao itapigwa Arusha.

Taarifa hiyo ya TPLB, inasema maombi hayo ni kwa mujibu wa kanuni ya 9 (7) ya Ligi Kuu inayotoa nafasi kwa timu kuchagua kucheza mechi zake mbili za nyumbani katika viwanja vingine miongoni mwa visivyokuwa na michezo ya Ligi.

“Bodi ya Ligi imekubali maombi hayo na tayari imefanya mawasiliano na wahusika wote wa mchezo huo kwa ajili ya taratibu za maandalizi,” ilisema taarifa hiyo.

Msimu uliopita KMC iliipeleka Yanga CCM Kirumba, huku Polisi Tanzania nao wakiipeleka Simba jijini humo na JKT Tanzania iliyoshuka daraja, ilipeleka mchezo wao mmoja mjini Iringa. Klabu zimekuwa zikieleza kwamba sababu kubwa ya kubadili viwanja ni kupata fedha nyingi wakilenga upepo wa mashabiki wao kwenye viwanja hivyo vya mikoani.