Uko hapa: NyumbaniMichezoMpira wa Miguu2021 07 19Article 547471

Soccer News of Monday, 19 July 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Yanga: Simba hawachomoki Kigoma

Yanga: Simba hawachomoki Kigoma Yanga: Simba hawachomoki Kigoma

YANGA mzuka umepanda, kwani unaambiwa wakati Nahodha Lamine Moro akirejeshwa kikosini, msaidizi wake Bakari Mwamnyeto na wenzake kambini wamesisitiza Simba hawachomoki Kigoma, kwani wanalitaka taji la ASFC kuendeleza ubabe kwa watani wao.

Mabosi wa Yanga umeamua kumalizana na beki huyo wa kati, huku kipa Metacha Mnata akimaliza adhabu yake jana na wote walisafiri na timu kwenda Dodoma kwa mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Bara uliopigwa jana kabla ya kujumuika katika kikosi kwenda Kigoma.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli aliliambia Mwanaspoti, Mghana huyo aliyekuwa amesimamishwa na Michael Sarpong pamoja na Metacha kwa utovu wa nidhamu ishu yao imeshamalizwa na Kocha Nasreddin Nabi na wapo huru kulingana na mahitaji ya kocha huyo.

“Adhabu ya Metacha aliyesimamishwa baada ya mechi na Ruvu Shooting inamalizika kesho (leo Jumapili), hivyo watarajie kukutana naye Kigoma kwenye ASFC, lakini juu ya Lamine, tofauti yao na Kocha Nabi imemalizika kama ilivyo kwa Sarpong, ingawa yeye hajajiunga na timu,” alisema.

Lamine alikuwa kwenye mechi y derby wakati Simba ikilala Machi 8 mwaka jana na ile ya sare ya 1-1 Novemba pamoja na ile waliopigwa 4-1 katika nusu fainali ya ASFC.

Juu ya taarifa kuwa Sarpong amepewa mkono wa kwaheri, Bumbuli alisema hana taarifa hizo isipokuwa anajua tofauti yake na Nabi ilishamalizwa, japo hajajiunga na timu. kama akitokea hata leo atajumuishwa kikosini kwani bado ni mchezaji wao.

“Sarpong bado hajarudi kazini, ila alishasamehewa, kuhusu kupewa baibai sijajua, kama lipo, litawekwa wazi, mbona Haruna Niyonzima mashabiki wamejua anaondoka?”

MZUKA KAMBINI

Aidha nahodha msaidizi wa Yanga, Mwamnyeto alisema kambini kwao mzuka upo juu kwa jinsi walivyopania na kujipanga kwa mchezo wa fainali ya ASFC mjini Kigoma, akitamba Simba isitarajie kutoka salama Lake Tanganyika.

Mwamnyeto alisema timu nzima imejiwekea malengo ya kuchukua kombe hilo baada kukosa la Ligi Kuu mbele ya Simba, hivyo Kigoma lazima kitaeleweka.

“Tumekosa ubingwa wa Ligi Kuu sasa tunajipanga kuchukua la ASFC ambalo tutacheza na Simba kule Kigoma. Tunajua itakuwa ni mechi ngumu kwetu, lakini kama timu tumejipanga kupambana hadi dakika ya mwisho ili tubebe kombe hilo,” alisema Mwamnyeto na kuongeza;

“Simba ni watani wetu wa jadi na wamekuwa wakionyesha ushindani kila tukutana nao, huwa tunashinda na tutaendelea kushinda hata Kigoma, kwani tunataka heshima iendelee.”

Licha ya Simba kubeba ubingwa, imekwama kupata ushindi mbele ya Yanga katika Ligi Kuu kwani imeambulia sare ya 1-1 mechi ya Novemba 7 mwaka jana na kulala 1-0 wiki mbili zilizopita na Januari 13 walipasuka kwa penalti katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2021 na mchezo huo wa Jumapili ijayo utakuwa wa nne kwa msimu huu.

Juu ya msimu huu unaoisha leo kwa timu yao kucheza na Dodoma Jiji, Mwamnyeto alisema ulikuwa mgumu, ila kwa maboresho yanayoendelea kufanyika Jangwani anaamini msimu ujao watakuwa moto maradufu.

“Huu ulikuwa msimu bora kwetu, licha ya changamoto nyingi. Nashukuru tunaenda kumaliza salama na tunaimani msimu ujao tutafanya vizuri zaidi ya hapa tulipoishia msimu huu,” alisema.