Uko hapa: NyumbaniMichezoMpira wa Miguu2021 07 16Article 547150

Soccer News of Friday, 16 July 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Zuchu atangaza balaa Zanzibar

Zuchu atangaza balaa Zanzibar Zuchu atangaza balaa Zanzibar

Dar es Salaam. Msanii aliyesaini na lebo ya WCB mwaka mmoja uliopita Zuchu ametangaza kufanya tamasha kubwa ‘Zuchu Home Coming’ litakalofanyika Agosti 21 mwaka huu katika visiwa vya Unguja huko Zanzibar.

Zuchu ameyasema hayo leo Julai 15, 2021 katika mkutano wake na vyombo vya habari alioufanya visiwani humo.

“Tangu nimeachiwa rasmi na WCB nimekuwa na shauku kubwa ya kutaka kufanya shoo ambayo itaonyesha nia na dhumuni la sanaa ninayoifanya,” amesikika msanii huyo.

Zuchu alisema sababu iliyomfanya kwenda kufanya tamasha hilo Zanzibar ilitokana na tamasha lake la kwanza alilolifanya katika ukumbi wa Mlimani City ‘I am Zuchu’ kuwa kubwa na lililovutia watu wengi.

“Taswira ya sanaa yangu ilichukuliwa tofauti baada ya mimi kutoka pale Mlimani City kuperfom shoo kubwa sana, nikasema safari hii sitaenda mkoa wowote nitarudi nyumbani ili hili jambo likaanzwe nilipotokea.

“Wote tunafahamu kwenye utafutaji unaweza kuishi popote lakini hii hainibagui kwamba mimi ni Mtanzania lakini nimetokea Zanzibar na nimekulia hapa,” amesema Zuchu.

Mkali huyo wa wimbo Sukari, ametaja sababu za kuita tamasha lake ‘Zuchu Home Coming’ kwamba ameita hivyo kwa kuwa anarudi nyumbani lakini pia anaamini mcheza kwao hutunzwa.

Amesema mwitikio mkubwa wa nyumbani ndiyo utawashtua wengi ambao hawamjui na wanataka kumfahamu.

Zuchu amsema kwenye tamasha hilo atapenda kushiriki na wasanii asilimia kubwa wanaotokea Zanzibar kwa kuwa wana uwezo na haki ya kushiriki katika tamasha hilo.

“Nimeongea nao na wameonyesha ushirikiano mkubwa sana, siku hiyo itapambwa na ngoma, benbati, vidumbaki, taarabu za zamani na za sasa lakini pia Zenj fleva ya zamani na sasa.

“Tutakuwa na wasanii wenzangu kutoka Bara ambao mnawajua, nia na dhumuni kubwa ni kushirikiana na wenzangu naamini hakuna cha mmoja kinachofanikiwa kwa ukubwa cha wengi kinafanikiwa kwa ukubwa,” amesema msanii huyo.

Aidha Zuchu aliwashkuru wasanii wenzake wa Zanzibar kwa kumpokea vizuri na ushirikiano waliomuonyesha tangu alipowaomba kushiriki katika tamasha lake Agosti 21 kwenye uwanja wa Amani.

“Tunatangaza rasmi Zuchu Home coming shoo na Zantel, narudi nyumbani nina shauku kubwa ya kuwaonyesha tulichojiandaa nacho nitoe shukrani za dhati kwanza kwa Zantel mimi balozi wao wa pasua anga campaign.”

Zuchu aliipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kumuunga mkono na kuwa naye bega kwa bega kupitia wizara mama za Mambo ya kale na utalii, Baraza la Sanaa Zanzibar na Wizara ya Sanaa na Utamaduni Zanzibar.

Ametaja viingilio katika tamasha hilo kuwa ni pamoja na viti maalum Sh30,000  na ambao watanunua kupitia mtandao wa Zantel itakuwa ni Sh29,000,  daraja la pili Sh5000 kwa kawaida ukinunua kwa Zantel utaipata kwa Sh4500 na daraja la kawaida Sh3000 na kwamba tamasha hilo litaanza mchana.

Katika upande mwingine Zuchu amesema tamasha hilo likawe chachu ya maendeleo kwa Zanzibar kitalii, kisanaa, kiukuaji wa biashara, ikainue hamasa kwa wasanii wa Zanzibar.

Pia amesema Julai 24 kutakua na semina kwa wasanii kujifunza mambo mbalimbali ya tasnia jinsi gani wanatakiwa kutumia mitandao ya kijamii kuwaingizia kipato, semina itakayotolewa nma wataalamu wa masuala ya sanaa.