Uko hapa: NyumbaniNchiPeopleMichezoTheogeness Kashasha

Watu Maarufu Tanzania

Michezo

Theogeness Kashasha

MCHAMBUZI MAHIRI WA MPIRA WA MIGUU

Kashasha Pc Data
Tarehe ya Kuzaliwa:
1957-11-17
Mahali pa Kuzaliwa:
Kagera
Date of Death:
2021-08-19
DECEASED

Kuzaliwa

Jina lake kamili ni Theogeness Alexander Kashasha ama anatambulika na wengi kama "Mwalimu Kashasha".

Mwalimu Kashasha alizaliwa 17 /11/1957, huko Maruko (Wilaya ya Bukoba Vijijini), Mkoani Kagera na katika Familia ya Mzee Alexander Kashasha yeye ni mtoto wa tano kati ya watoto kumi.

Elimu

Alianza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Kabanga na alihitimu katika Shule ya Msingi kabale huko huko kagera.

Aliendelea na Masomo ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Shirati na akahitimu mwaka 1976 ambapo alijiunga na mafunzo ya Ualimu katika Chuo cha Ualimu Songea.

Mwaka 1987 mpaka 1989 alisomea elimu ya Physical Education katika chuo cha Ualimu kilichopo Butimba Mkoani Mwanza na akajiendeleza katika taaluma hiyo mpaka akapata Shahada ya juu katika Chuo Kikuu cha Da es Salaam.

Mwaka 2005 Mwalimu Kashasha aliamua kujiendeleza kimasomo na kupata Stashada ya Adult Education Community Development, Lakini Mwalimu Kashahsha katika enzi za Uhai wake alifanikiwa kuhudhuria kozi fupi fupi na kutunukiwa vyeti kama Federation African de Football, Olympic Solidarity Coaching Course na Pia Physical Education and Sports for Service tutorials.

Lakini pia Mwalimu Kashasha alitunukiwa cheti cha heshima kutoka klabu ya Pamba FC.

Kazi

Mwalimu Kashasha alikuwa mtumishi wa Serikali kuanzia mwaka 1986 mpaka mwaka 2017 alipostaafu wakati akiwa katika Chuo cha Ualimu Vikindu.

Wakati wa Utumishi wake mwalimu kashasha alifanya kazi katika Halmashauri mbali mbali kama vile Halmashauri ya Bunda, Musoma na Chuo cha Ualimu Korogwe.

Baada ya Kustaafu rasmi kwa mujibu wa Sheria (2017) Mwalimu Kashasha aliendelea kufanya kazi na Shirika la utanzaji Tanzania (TBC) kama mtangazaji wa vipindi vya michezo na Mchambuzi wa mpira wa miguu.

Mwalimu Kashasha pia amefanya kazi kama Mshauri katika Shule za Fountain Gate Academy.

Alifikaje TBC ?

Mwalimu alianza Uchambuzi TBC mwaka 2014 wakati akiwa ni mkufunzi wa taaluma na michezo katika chuo cha Ualimu Vikindu.

Na kupelekwa kwake kulitokana na wachambuzi wengi wa Mpira waliokuwa wakifanya kazi TBC kutodumu hivyo katika majadiliano viongozi wakakubaliana wamlete yeye baada ya kupendekezwa jina lake na aiewahi kuwa Mwanafunzi wake Jesse John.

Jesse John ndio alietoa wazo la kumleta Mwalimu kashasha kwa kuwa alikua akimfahamu tangu miaka ya Themanini mwishoni, wakati akisoma Chuo cha Ualimu Butimba Mwanza na aliwahi kumfundisha akiwa golikipa wa timu ya Chuo.

Utaalamu katika Soka

Mwalimu Kashasha alianza kucheza soka tangu akiwa mdogo akimudu nafasi ya kiungo mshambuliaji, yaani namba nane na 10 kiasi cha kubatizwa jina la Pele kutokana na jinsi alivyokuwa mahiri katika eneo hilo.

Mbali na kucheza soka, Kashasha pia alikuwa mwalimu kitaaluma wa mchezo huo aliyesomea sayansi ya Michezo katika Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza ambako ndiko alikokutana na Waziri Mkuu na kutengeneza timu tishio, kisha alitua Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikohitimu Shahada ya Sayansi ya Michezo.

Kashasha alifundisha shule mbalimbali na vyuo vya Ualimu katika masuala ya michezo, hususan soka kabla ya kujifunza kozi tofauti za ukocha kisha akafundisha timu kadhaa na kuibua vipaji mbalimbali.

Mojawapo ya vipaji vilivyowahi kunolewa na Kashasha ni Paul Rwechungura, kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na timu ya Pamba anayeishi nchini Marekani, Riziki Mchumila na Nico Bambaga aliowanoa ndani ya timu ya Mkoa wa Mara.

Katika mahojiano enzi za uhai wake, Kashasha aliwahi kusema amewahi kucheza pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambapo yeye alizungusha dimba la juu na Majaliwa akikipiga winga ya kulia.

Pia alisoma kozi mbalimbali na makocha maarufu nchini kama Sunday Kayuni, Charles Mkwasa na Mohammed Adolf Rishard.

Mahusiano yake kazini

Mwalimu Kashasha anazungumzwa kama alikua ni rafiki, zaidi ya baba, Mshauri kwa kuwa alipenda kuona kila mtu anafanya vizuri katika eneo analolipenda hakusita kumuita mtu na kumpa ushauri.

Mwalimu Kashasha ni mtu ambae ameleta misemo mingi ya upekee katika utangazaji wake wa mpira wa miguu na namna anavyouchambua mpira wa miguu.

Familia

Mwalimu Kashasha alifunga ndoa na Elizabeth Samwel mwaka 1995 katika Kanisa la Mtakatifu Joseph na walibarikiwa kupata watoto wawili, Theosina na Theopista.

Hivyo ameacha mjane na watoto wawili.

Kifo chake

Mwalimu Alex Kashasha alianza kusumbuliwa na Presha tangu 12/3/2021, ambapo alikua akipata matibabu katika hospitali ya Tumaini Kongowe.

Baada ya Vipimo iligundulika Mwalimu Kashasha anasumbuliwa na tatizo la Figo na kuhamishiwa katika Hopsitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi na alikua akihudhuria Clinic na hali yake ilikaa vyema .

4/8/2021 hali yake ilibadilika ghafla na kupelekea kulazwa katika Hospitali ya Kairuki Jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili na siku ya tarehe 19/8/2021 majira ya saa saba mchana , Mwalimu Kashasha alifariki dunia akiwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi .

Mwalimu Kashasha amezikwa Jumatatu ya Agosti 23, 2021 katika Makaburi ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.

Mitandao