Uko hapa: NyumbaniNchiPeopleMichezoZacharia Hans Poppe

Watu Maarufu Tanzania

Michezo

Zacharia Hans Poppe

Mfahamu Hans Poppe

Popee
Tarehe ya Kuzaliwa:
N/A
Mahali pa Kuzaliwa:
Dar es salaam
Date of Death:
2021-09-10
DECEASED

Jina lake kamili ni Zacharia Hans Poppe, ambaye alizaliwa mwaka 1956 Jijini Dar es Salaam na kukulia Mkoani Iringa.

Hans Poppe ni Chotara wa Kijerumani na Tanzania. Baba yake alikua ni raia wa Ujerumani na mama yake ni Mhehe wa Ipogoro lringa. Baba yake, Mzee Hans Poppe, alikua ni RPC wa Mkoa wa Ziwa Magharibi (sasa Kagera). Aliuawa na majeshi ya Idi Amin 1971, Mtukula, Kagera.

Baada ya kumaliza elimu ya Sekondari, Zacharia alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambako alifikia cheo cha Kapteni, kabla ya kuachishwa kazi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, kwa tuhuma za uhaini, dhidi ya serikali ya awamu ya kwanza ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwaka

Lakini mwaka 1995, Zacharia aliachiwa huru kwa msamaha wa Rais wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, mwezi mmoja kabla hajamuachia Ikulu ya Tanzania, Benjamin William Mkapa, Rais wa awamu ya tatu.

Kama zinavyosema sheria za nchi, mtu aliyehukumiwa kifungo, hana haki ya kugombea wadhifa wowote au kuajiriwa tena, Zacharia naye hakuweza kurejea kazini, badala yake akaamua kujiajiri, kwa kuanzisha miradi yake mwenyewe, ikiwemo kampuni ya usafirishaji ZH Poppe.

HANS POPE NA SIMBA SC Zakaria Hans Poppe ni Binadamu mtiifu kupita maelezo linapokuja suala la Klabu ya Simba SC.

Alianza kuipenda Simba SC mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na zaidi mwenyewe anasema, mechi ambayo ilimfanya ajitamke rasmi yeye ni Simba damu ilikuwa dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga Juni 23, mwaka 1973, ambayo Wekundu wa Msimbazi, walishinda 1-0, bao pekee la Haidari Abeid ‘Muchacho’ dakika ya 68.

“Nakumbuka ilikuwa ni ligi ya mtoano, tuliitoa Yanga tukaenda hadi kuchukua ubingwa kwa kuwafunga Lake kule Kigoma, kipindi kile Simba ilikuwa inaundwa na vijana wadogo wadogo tu, ilikuwa raha sana". aliwahi kusema Hans Poppe katika moja ya mahojiano yake.

Ni Simba ambayo mwaka 1974 iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kuchukua hili Kombe ambalo linaitwa la Kagame, wakati huo linaitwa la Afrika Mashariki na Kati na pia ilifika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), tukatolewa kwa fitina na Waarabu(MehallaELKubra),”aliwahi kukumbusha Zacharia.

Zacharia aliendelea kuwa mpenzi wa Simba, hadi baadaye akaamua kuwa mwanachama.

Lakini siku zote alikuwa pembeni, hadi lilipoundwa kundi la Friends Of Simba ndipo akaamua kujiunga nalo, ili naye aweze kutoa michango yake zaidi.

Wakati wa uongozi wa Mwenyekiti, Hassan Dalali ambao ulionekana kuelemewa na majukumu ya timu, ndipo alipata umaarufu zaidi ndani ya Simba, kutokana na kusaidia zaidi.

Uongozi wa Dalali baada ya kugundua umuhimu wake ukaamua kumpa jukumu la kusimamia fedha na alifanikiwa kudhibiti fedha na kuanzisha mpango wa kuiwezesha klabu kujitegemea katika mambo mbalimbali, ikiwemo suala la usajili badala ya kutembeza kablu.

Anasema kutokana na kufanya vizuri katika jukumu hilo, wengi miongoni mwa wanachama na viongozi wa Simba wakamuomba agombee Uenyekiti.

“Lakini siku zote kuna kitu kilikuwa kinanipa shida. Nilikuwa sijui ni msamaha wa aina gani niliopewa na Rais, unajua Rais anaweza pia kutoa msamaha wa kufuta na kosa pia,”alisema Hans Pope katika moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari “Lakini nilijaribu sana kufuatilia ili kujua aina ya msamaha wangu, nilikwenda hadi Magereza, lakini hawakunipa jibu, mwishowe nikaamua kuacha tu, sasa nilipojaribu kuomba uongozi Simba, ndipo TFF wakatumia kipengele cha mimi kuwahi kufungwa kuniengua,”

Hata hivyo, Zacharia alisema kwamba umefika wakati sheria hiyo irekebishwe kwa mtu anayetoka jela awekewe muda maalum wa kuzuiwa kushiriki katika madaraka na ajira, kabla ya kuruhusiwa kurejea kwenye maisha ya kawaida.

“Unajua mtu anapofungwa lengo ni kumfundisha, ili baadaye akirudi uraiani awe raia mwema, sasa haiwezekani arudi uraiani halafu amewekewa vipingamizi, mimi naamini ipo haja ya kurekebisha hii sheria,”anashauri Zacharia.

Zacharia Hans Poppe pamoja na kuukosa Uenyekiti, alipata fursa ya kuendelea kuisaidia klabu yake,baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili.

NINI JUKUMU LA KAMATI YA USAJILI YA SIMBA? Zacharia na Kamati yake hupokea mapendekezo kutoka kwa Kamati ya Ufundi juu ya aina ya wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa, ndipo wao hutafuta wachezaji.

Kwanza, Kamati ya Ufundi inakuwa imekutana na benchi la ufundi, imepewa ripoti ya kitaalamu, wanajadiliana ndio wanatuletea orodha ya wachezaji wanaotakiwa kwa maana ya nafasi zao.

Sasa sisi tunakwenda kufanya tathmini ya wachezaji gani bora ndani na nje ya nchi, tukiwapata, tunarudi kwa Kamati ya Ufundi, tunawapa majina, sasa wao ndio wanakwenda kuwafuatilia uwezo wao na wakiridhika, wanatupa jibu, sisi ndio tunawasaini,”anasema.

Kwa mujibu wa Zacharia Hans Poppe aliwahi kusema kwamba hakuna mtu anayesajili kwa fedha zake Simba SC, bali ni fedha za klabu.

“Sisi Kamati ya Usajili tunapotaka kumsajili mchezaji, tunakwenda kwa Kamati ya Fedha, sasa wao ndio wanatuambia uwezo wao unafikia wapi, pale ambako pamezidi sasa tunatoka tunakwenda kuchangishana na ndugu zetu Friends Of Simba na wadau wengine tunamalizana na mchezaji,” aliwahi kunukuliwa HansPoppe.

MIZOZO NA SERIKALI Mwaka 2018 Hans Poppe aliingia matatani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) baada ya kushutumiwa kutoa taarifa ya uongo kwa mamlaka ya mapato TRA ili alipe kodiambayo si stahiki.

Zakaria alitoa taarifa kwa TRA kuwa Simba SC imenunua nyasi bandia kutoka China kwa dola za kimarekani 45,577 sawa na pesa za kitanzania Tsh milioni 105 kumbe uhalisia nyasi zilinunuliwa kwa dola za Kimarekani 109,499 sawa Tsh milioni 252 hivyo TAKUKURU ikatafsiri kuwa hakua na nia ya kulipa mapato stahiki kwa serikali .

NINI DUKUDUKU LAKE KATIKA SOKA Vurugu katika usajili na uendeshaji soka kwa ujumla, ni vitu ambavyo Zacharia hataki hata kuvisikia. Aliwahi kutolea mfano Yanga walivyofanya kwa beki wa APR ya Rwanda, Mbuyu Twite, kwamba hayo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati.

“Mwenzako amekwishazungumza na mchezaji, wewe huna sababu ya kwenda kuzungumza naye na kumrubuni, kupandisha dau, hayo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati.

KAMA MWANAMICHEZO , HANS POPPE NI SHABIKI WA TIMU ZA ULAYA Hans Poppe alikua ni Shabiki wa Arsenal pale England, Bayern Munich pale Ujerumani na Barcelona kwa Hispania. Kwa upande wa wachezaji alimuhusudu Alex Song, Robin van Persie na Frank Ribbery.

FAMILIA Japo hajaiweka wazi sana lakini Zacharia Hans Poppe ni Baba wa watoto tisa, watoto ambao amewapata kutoka kwa wanawake wanne tofauti.

UMAUTI Takribani wiki moja na nusu iliyopita , Kituo kimoja cha Redio kiliwahi kumpigia simu Hans Poppe alipopokea akadai yuko hospitali anaumwa hivyo anapatiwa matibabu.

Lakini Septemba 10 Majira ya Jioni taarifa za kifo chake zilisambaa na kuhitimisha Safari ya Mwanamichezo , Shabiki na Mwanachama wa kutupwa wa Simba Sports Club.

Mpaka umauti unamkuta katika Hospitali ya Agha Khan Jijini Dar es Salaam, Zacharia Hans Pope alikua ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC.

TanzaniaWeb